IQNA

Iran yalaani vikali mlipuko wa Beirut, Lebanon

9:00 - December 29, 2013
Habari ID: 1348030
Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani mripuko wa kigaidi uliotokea huko Beirut mji mkuu wa Lebanon.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imelaani mlipuko wa kigaidi uliotokea leo huko Beirut ambao umepelekea kuuliwa shahidi na kujeruhiwa raia kadhaa wa nchi hiyo akiwemo Muhammad Shatah Waziri wa Fedha wa zamani wa Lebanon. Katika taarifa yake hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetoa mkono wa pole kwa serikali, wananchi na familia za wahanga na majeruhi wa mlipuko huo wa kigaidi na kusisitiza juu ya udharura wa kutambuliwa na kuadhibiwa mara moja wale wote waliohusika na jinai hiyo.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeongeza kuwa wananchi wa Lebanon, viongozi na makundi ya kisiasa ya nchi hiyo kama ilivyokuwa huko nyuma watafanikiwa kuzishinda njama za Wazayuni na vibaraka wao wa ndani na kieneo kwa kulinda umoja miongoni mwao na kuwa macho. Imesema mlipuko huo ni sehemu ya oparesheni za kigaidi zilizoendelea katika  miezi ya hivi karibuni kwa lengo la kuvuruga amani na utulivu wa Lebanon na kuzusha fitna miongoni mwa raia wa nchi hiyo.

Muhammad Shatah Waziri wa Fedha wa zamani wa Lebanon ameuawa katika mripuko mkubwa uliotokea leo asubuhi karibu na hoteli ya Phoenicia huko Beirut mji mkuu wa Lebanon. Duru za hospitali na Jumuiya  ya Msalaba Mwekundu ya Lebanon zimeripoti kuwa watu wanane wameuawa na wengine 70 wamejeruhiwa katika mripuko huo wa leo huko.

Wakati huohuo Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Lebanon amesema kuwa kuuliwa Waziri wa zamani wa Fedha wa Lebanon katika mripuko wa kigaidi wa leo huko Beirut kumetekelezwa kwa ajili ya kufanikisha maslahi na malengio haramu ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Ghazanfar Rokniabadi amesema kuwa wale wote waliotekeleza kitendo hicho cha kigaidi wamekusudia kuzusha fitna nchini Lebanon na katika nchi nyingine za Mashariki ya Kati ili kutimiza malengo yao machafu.

1347585

captcha