IQNA

HRW: Katili Sharon alipaswa kushtakiwa

9:12 - January 14, 2014
Habari ID: 1358687
Shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch limesema ni aibu kuwa waziri mkuu wa zamani wa utawala haramu wa Israel Ariel Sharon amekufa pasina kufikishwa kizimbani kujibu mashtaka ya kuhusika na mauaji ya kinyama ya Sabra na Shatila.

Itakumbukwa kuwa mnamo mwezi Septemba 1982, wanajeshi wa utawala haramu Israel, wakiongozwa na Ariel Sharon ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Vita, walishambulia kambi za wakimbizi wa Kipalestina za Sabra na Shatila karibu na mji kuu wa Lebanon, Beirut na kupelekea takribani Wapalestina 3,500 hadi 5,000 kuuawa shahidi wakiwemo wanawake, wazee na watoto wadogo.

Mkuu wa Human Rights Watch Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika Sarah Leah Whitson aidha amelaani nafasi ya Sharon katika mauaji ya kiongozi wa Palestina Yasser Arafat mwaka 2004. Amesema Sharon alikuwa mtenda jinai za kivita ambaye alipaswa kufikishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC. Wakati huo huo Wapalestina wanaendelea kusherehekea kifo cha Sharon ambaye alipewa jina la 'chinjachinja wa Sabra na Shatila' kutokana na ukatili wake. Sharon ambaye alikuwa kwenye koma tokea mwezi Januari mwaka 2006 baada ya kupatwa na mshituko wa ubongo, alikufa Jumamosi akiwa na umri wa miaka 85.

Ukweli wa mambo ni kuwa, umri wa Sharon ulikuwa umefikia tamati tangu Januari mwaka 2006 baada ya kupata mshituko wa ubongo na aliyendelea kuishi katika koma kwa msaada wa vifaa vya kitiba. Wazayuni walikuwa wamempatia Sharon lakabu ya buldoza wakikumbuka masiku ambayo Sharon alikuwa Waziri wa Kilimo na kwa amri yake nyumba za Wapalestina zikibomolewa na mashamba yao kuharibiwa ili nafasi yake kujengwe vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi. Hata hivyo Wapalestina kwa upande wao wanamtambua katili Sharon kwa jina la "chinjachinja" wakikumbuka kipindi ambacho Sharon alikuwa Waziri wa Vita wa Israel na kwa amri yake Lebanon ikakaliwa kwa mabavu na kilichofuatia ni kuuawa kwa umati Wapalestina katika kambi za wakimbizi za Kipalestina za Sabra na Shatila katika viunga vya Beirut mwaka 1982 na kwa muktadha huo ulimwengu ukakumbwa na msiba na majonzi makubwa. Historia itahifadhi milele tukio chungu la maafa ya Sabra na Shatila kwani katika tukio hilo, zaidi ya wanawake, watoto, vijana na wazee wa Kipalestina elfu mbili waliuawa kwa umati na mamluki wa kifalanja wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Kama vile haitoshi, ukatili wa mafalanja na Wazayuni ulidhihiri zaidi pale walipoamua kucheza na kunengua mbele ya maiti za Wapalestina walizoziua kinyama. Kwa hakika mauaji ya Deir Yassin, Kafr Qasim na Sabra na Shatila ni miongoni mwa maafa ya kutisha kabisa katika karne ya 20 ambayo hayatasahauliwa. Mwaka 1982, Sharon akiwa Waziri wa Vita wa utawala haramu wa Israel aliongoza vita dhidi ya Lebanon na mwaka 1983 alikabiliwa na mashanikizo makubwa ya fikra za waliowengi ulimwenguni kutokana na mauaji yake ya umati dhidi ya Wapalestina katika kambi za wakimbizi wa Kipalestina za Sabra na Shatila na hivyo akauzuliwa kutoka katika wadhifa wake huo. Hata hivyo Sharon alichomoza tena katika uga wa siasa za Israel mwaka 1990 akiwa Waziri wa Nyumba na kufanikiwa kujenga nyumba laki moja na arobaini na nne elfu katika maeneo ya Wapalestina kwa ajili ya walowezi wa Kiyahudi na kutokana na sababu huyo akapewa lakabu ya "Baba wa Harakati ya Ujenzi wa Vitongoji vya Walowezi wa Kizayuni." Katika uga wa siasa, Sharon ni mwasisi pia wa vyama viwili vya mrengo wa kulia vya Likud na Kadima. Mwaka 1998 Sharon akawa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Israe na mwaka 2000 aliingia katika Msikiti wa al-Aqswa na kulivunjia heshima eneo hilo takatifu, kitendo ambacho kilizua hasira na ghadhabu za Wapalestina na kupelekea kutokea Intifadha ya Pili. Mnamo mwaka 2001 Sharon akawa Waziri Mkuu wa Israel. Katika kipindi cha kuwa kwake Waziri Mkuu, chinjachinja huyo wa Sabra na Shatila aliongoza mpango wa ujenzi wa ukuta wa kibaguzi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan lengo likiwa ni kupora zaidi ardhi za Wapalestina.  Kifo cha Ariel Sharon kimepelekea kufungwa faili jingine la mwasisi wa kukaliwa kwa mabavu Palestina.

1353554

captcha