IQNA

UN yataka uchunguzi kuhusu mauaji ya Waislamu Myanmar

12:17 - January 26, 2014
Habari ID: 1366482
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Navy Pillay ametaka kufanyike uchunguzi kamili wa mauaji hayo na kuhakikisha kwamba uadilifu unatendeka.

Umoja wa Mataifa umeripoti kuwa tarehe 9 na 13 Januari Mabudha wenye misimamo mikali walivamia maeneo ya Waislamu katika jimbo la Rakhine na kuua kwa umati makumi ya Waislamu. Ni kwa msingi huo ndio Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa akataka kufanyike uchunguzi. 

Vilevile jumuiya ya kutetea haki za binadamu ya Fortify Rights imetoa ushahidi wa watu walioshuhudia na nyaraka za kuaminika zinazothibitisha kuwa Waislamu wasiopungua 40 waliuawa kwa umati katika shambulizi lililofanywa na askari usalama wa serikali ya Myanmar kati kati ya mwezi huu wa Januari kwenye jimbo la Rakhine.

Kwa miaka mingi Waislamu wanaounda jamii ya waliowachache wa Myanmar wamekuwa wakisumbuliwa na ubaguzi wa aina mbalimbali kutokana na kunyimwa haki zao za kiraia na kijamii. Hata hivyo tangu miaka miwili iliyopita ukatili na unyama huo umeongezeka sana. Suala hili limezifanya taasisi na jumuiya nyingi za kimataifa za kutetea haki za binadamu kuilaumu serikali ya Myanmar kwa kufumbia macho na kukanyaga haki za Waislamu nchini humo.

Baadhi ya viongozi wa nchi ya Myanmar yenye jamii ya watu milioni 60 waliahidi mwaka 2011 baada ya kuhitimishwa utawala wa kijeshi ulioitawala nchi hiyo kwa miaka mingi kwamba watafanya marekebisho. Hata hivyo badala ya marekebisho hayo, Waislamu sasa ndio wanaofanywa wahanga wakubwa wa ukatili na mauaji ya kizazi na wanaobakia hai wanalazimika kukimbia, kufungiwa katika kambi za lazima na wanawake na wasichana kufanywa watumwa wa ngono katika kambi za jeshi. Suala hilo ni kengele ya hatari kwa jamii ya kimataifa ambayo inalazimika kuchukua hatua za dharura za kukomesha hali hiyo na kuokoa maisha ya Waislamu nchini Myanmar.

1365835

captcha