Taarifa kutoka Bangui mji mkuu wa nchi hiyo zinasema kuwa, Daktari Joseph Kalite alipoteza maisha baada ya kushambuliwa na wanamgambo wa Kikristo wakati akitoka Msikiti Mkuu ulioko mjini Bangui. Shambulio hilo limetokea ikiwa imepita siku moja tu, tokea Bi. Catherine Samba – Panza Rais wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya Kati kuyataka makundi yanayobeba silaha kuweka chini silaha zao. Wakati huohuo, Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binadamu la Amnesty International limeripoti kwamba, kwa akali Waislamu 50 wameuawa baada ya wanamgambo wa Anti Balaka kushambulia vijiji viwili kaskazini magharibi mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Wiki iliyopita, wanamgambo wa Kikristo pia waliwauwa Waislamu 22, wakiwemo watoto watatu na kuwajeruhi makumi ya wengine. Shirika hilo limeeleza kuwa, vikosi vya kimataifa vya kulinda amani nchini humo vimeshindwa kuilinda jamii ya Waislamu na mashambulizi yanayofanywa na Kikristo dhidi yao. Imeelezwa kuwa, mapigano ya kidini kati ya Waislamu na Wakristo yamepelekea kuuawa watu wasiopungua 2,000 kufikia Disemba mwaka jana, na zaidi ya watu milioni moja kuyahama makazi yao.
Wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wanaituhumu Ufaransa ambayo ni mkoloni wa zamani wa nchi hiyo kuwa inachochea mapigano hasa uhasama baina ya Waislamu na Wakristo nchini humo. Jamhuri ya Afrika ya Kati ni nchi yenye umuhimu mkubwa kwa madola makubwa ulimwenguni kutokana na kuwa kwake katika kitovu cha bara la Afrika. Nchi hiyo inakodolewa jicho la tamaa na nchi kubwa duniani kutokana na utajiri mkubwa wa maliasili za madini kama almasi, urani na dhahabu.