Rais Rouhani ameongeza kuwa iwapo kutakuwepo irada imara katika upande wa pili wa mazungumzo ya nyuklia na Iran, basi kuna uwezekano wa kufikiwa mapatano ya mwisho na kamili katika kipindi cha muda mfupi. Rais Rouhani ameyasema hayo leo Jumanne mjini Tehran alipokutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan ambaye anaongoza ujumbe wa Taasisi ya Jopo la Wazee waliowasili nchini mapema Jumapili. Wanachama wa jopo hilo wanaoandamana na Annan ni pamoja na rais wa zamani wa Finland Martti Ahtisaari, Askofu Desmond Tutu wa Afrika Kusini na rais wa zamani wa Mexico Ernesto Zedillo. Akizungumza na wazee hao, Rouhani aliwabainishia kuwa, shughuli zote za nyuklia zinafanyika kwa malengo ya amani na zitabakia hivyo hivyo. Kwingineko katika matamshi yake, rais wa Iran alisema migogoro ya kieneo inatokana na umasikini wa kiutamaduni na kiuchumi, ukosefu wa uadilifu na demokrasia pamoja na kuwepo vikosi vya kigeni vinavyoingilia mambo ya eneo. Amesema kunahitajika umoja wa pande zote ili kukomesha vita na mauaji Syria. Kwa upande wake Annan amesema dunia inatakiwa kuutafutia suluhisho mgogoro wa Syria na kwamba majirani wa Syria na hasa Iran ina nafasi muhimu katika kutatua mgogoro wa nchi hiyo.