IQNA

Siku ya Kimataifa ya Hijab yaadhimishwa Nigeria

9:20 - February 02, 2014
Habari ID: 1369408
Wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Nigeria wameadhimisha Siku ya Kimataifa ya Hijab na kutangaza kufungamana kwao na Waislamu kote duniani katika kutetea haki ya wanawake Waislamu kuwa na uhuru wa kuvaa Hijabu.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Habari zaQur'ani IQNA, Jumuiya ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Nigeria imejiunga na Waislamu wengine duniani katika  Siku ya Kimataifa ya Hijabu ambayo huadhimishwa Februari Mosi. Akizungumza mjini Abuja, Hajia Hafsah Badru kiongozi wa wanafunzi wa kike katika Jumuiya ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Nigeria  amesema, 'Hijabu ni vazi la heshima na ni ngao ya mwanamke.' Wanawake Waislamu na wasiokuwa Waislamu jana waliandamana katika zaidi ya nchi 116  duniani kuunga mkono  vazi la  Hijabu.
Huu ni mwaka wa pili wa maadhimishi ya  Siku ya Kimataifa ya Hijabu ambayo ilipendekezwa ili kuwahimiza wasio kuwa Waislamu kuvaa Hijabu na ili waweze kufahamu ni kwa nini Waislamu huvaa vazi hilo la staha.
Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na wimbi kubwa la kupinga Hijabu katika nchi za Magharibi hasa nchini Ufaransa ambapo vazi hilo la Kiislamu limepigwa marufuku katika baadhi ya maeneo ya umma.
1369212

captcha