Baraza la Maulamaa nchini Bahrain linahesabiwa kuwa taasisi kubwa zaidi ya wananchi na Waislamu wa Madhehebu ya Kishia nchini humo, na tokea ilipoanzishwa harakati na mwamko wa wananchi tarehe 14 Februari 2011, limekuwa na nafasi muhimu ya kuziongoza harakati za wananchi dhidi ya utawala wa kifalme wa Aal Khalifa. Hatua ya utawala wa Aal Khalifa ya kuzivunja taasisi na jumuiya za Kiislamu nchini Bahrain inaonyesha jinsi utawala huo ulivyoshindwa kuishi kwa maelewano na wananchi wa Bahrain, na kudhihirisha mwenendo na muamala wake wa kidikteta na ukiritimba pamoja na hofu na kiwewe kikubwa kilichoupata utawala huo wa kiimla juu ya harakati zozote za wananchi zinazofanyika katika kalibu ya taasisi za Kiislamu.
Nyendo za utawala wa kifalme wa Aal Khalifa zinaonyesha kuwa, utawala huo licha ya kukandamiza uhuru wa kisiasa wa wananchi unawazuilia pia wananchi haki zao nyingine za kimsingi kama vile uhuru wa kuendesha harakati zao za kidini. Utawala wa Bahrain ulikuwa na mikakati ya kuziweka taasisi na jumuiya zote za kidini na za kiraia kuwa chini ya udhibiti wake na kuzuia harakati za taasisi na jumuiya hizo. Hii ni katika hali ambayo, taasisi kadhaa za kisheria na hali kadhalika mawakili wa Bahrain wameonyesha radiamali zao kuhusiana na amri hii isiyokuwa ya kiadilifu na usawa ya vyombo vya sheria vya utawala wa Aal Khalifa. Taasisi ya Haki za Binadamu ya Bahrain imetangaza kuwa, kuvunjwa Baraza la Maulamaa ni dhulma kubwa na inayochukiza mno.
Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa, harakati za Baraza la Maulamaa wa Kiislamu zilikuwa na shabaha ya kuinyanyua nafasi ya muqawama wa wananchi wa Bahrain, na kwamba hatua ya kuvunjwa baraza hilo bila shaka itaziumiza nyoyo za wananchi na hatimaye kuvurugika mwenendo wa mazungumzo ya kitaifa. Utawala wa Aal Khalifa uliyaita makundi ya upinzani kwenye mazungumzo ya kitaifa ili kuvuta muda, na wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, utawala huo umefanya hivyo ili kupunguza malalamiko na mashinikizo ya wananchi kwani hauna nia njema na ya dhati ya kufanya mazungumzo na wapinzani. Vitendo dhidi ya dini tukufu ya Kiislamu na vile vya uharibifu vinavyofanywa na utawala huo wa kifalme vya kubomoa makumi ya Misikiti tangu wakati zilipoanza harakati za wananchi wa Bahrain, vimewafanya walimwengu na hasa Waislamu wabaini uhakika huu kwamba utawala huo una ajenda za kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu kwa kuvamia maeneo na taasisi za kidini.
Utawala wa Aal Khalifa kila mara unakabiliana na mafundisho ya Kiislamu yanayokabiliana na sera za madola ya kibeberu, mafundisho ambayo yanaonekana kuwa ni kikwazo cha kuendelea kubakia madarakani utawala huo wa kidikteta. Kwa upande huo, utawala wa Aal Khalifa umeweka azma ya kulenga itikadi za Kiislamu za wananchi wa Bahrain na kuwalazimisha wananchi wazikubali siasa zake za kibeberu. Utawala huo unazibana harakati na shughuli za kidini, suala ambalo litawahamasisha zaidi wananchi waendelee kukabiliana na utawala huo usiokuwa wa kidemokrasia na kuandaa mazingira ya kuwepo utawala wa wananchi utakaofuata misingi ya kidini.
1368508