IQNA

Ayatullah Khatami:Marekani itajuta ikishambulia Iran

10:59 - February 02, 2014
Habari ID: 1369542
Khatibu wa muda wa Sala ya Ijumaa hapa mjini Tehran, Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami ametoa onyo kali kwa Rais Obama Marekani na kusema kuwa Marekani itathubutu kuishambulia Iran basi watajuta kosa lao hilo.

Ameongeza kuwa Iran itakabiliana vikali na yeyote mwenye nia ya kuhujumu ustaarabu, fahari na mafanikio ya taifa hili. Ayatullah Khatami amesema Wamagharibi daima wamekuwa wakilenga kuvuruga ustaarabu wa Kiislamu hapa nchini lakini kuwa macho Wairani dhidi ya njama hizo kumewafanya maadui kuangukia pua. Ayatullah Ahmad Khatami pia amezungumzia matamshi ya hivi karibuni ya viongozi wa Marekani akisema Iran inapaswa kujibu vitisho vya Washington kwa nguvu zote.
Juzi Jumatano Rais Barack Obama wa Marekani alisema kwenye hotuba yake ya kila mwaka kwamba, mashinikizo ya vikwazo na vitisho vya kutumiwa nguvu za kijeshi ndivyo vilivyoilazimisha Iran kwenda kwenye meza ya mazungumzo na nchi za 5+1. Pia jana Alhamisi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry alisema kuwa, Washington iko tayari kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya Iran iwapo Tehran itakiuka mkataba wa Geneva uliosainiwa Novemba 24.
Ayatullah Khatami amesema viongozi wa Washington wanapaswa kutambua kuwa, Iran ni nchi yenye nguvu na uwezo mkubwa wa kujilinda na kuwataka kukoma kutoa vitisho kama hivyo.
Khatibu wa muda wa Sala ya Ijumaa hapa mjini Tehran pia amezungumzia kadhia ya Syria akisema kukwama mazungumzo ya Geneva ni matokeo ya kutoishirikisha Iran kwenye mazungumzo hayo. Amesisitiza kuwa Iran ni sehemu ya dawa mujarabu kwa kadhia ya Syria na kuzidi kuachwa nje mitazamo ya Tehran kuhusu kuutatua mgogoro huo kutaifanya hali ya mambo iwe tete.
1368588

captcha