IQNA

Imam Khamenei: Marekani haiwezi kuuondoa Mfumo wa Kiislamu

11:25 - February 09, 2014
Habari ID: 1372874
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei amesema madola yanayoingilia masuala ya ndani ya nchi nyengine ni kikwazo kwa maendeleo na kujitawala nchi za eneo hili.

Ayatullah Khamenei ambaye pia ni amiri jeshi mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi Iran ameyasema hayo Jumamosi mbele ya hadhara ya makamanda, maafisa na askari wa jeshi la anga kwa mnasaba wa siku ya jeshi hilo na kueleza kwamba madola hayo yanayoingilia masuala ya nchi nyengine yanataka kuwafanya wananchi wa mataifa ya eneo waamini kwamba kujitawala kwao bila ya kuwa na utegemezi kuna mgongano na kupata maendeleo lakini maneno hayo ni potofu na yamebuniwa na madola hayo tu. Akibainisha maana ya kujitawala bila ya kuwa na utegemezi Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliashiria mbinu za Ukoloni Mamboleo za kuwatumia vibaraka wao badala ya kujiingiza moja kwa moja katika nchi na kufafanua kwamba katika kukabiliana na Ukoloni Mamboleo, mbali na kupambana na udikteta wa ndani unaotawala inalazimu kukabiliana pia na Ubeberu wa nje unaounga mkono udikteta huo, kwa sababu kupambana na udikteta tu na kisha kufanya muamala na Uistikbari hakutokuwa na tija yoyote. Katika sehemu nyengine ya hotuba yake, Ayatullah Khamenei amebainisha kuwa kutokuwa na utegemezi katika kujitawala maana yake si kususa na kuwa na muamala mbaya na nchi za dunia bali ni kujiwekea ngao na ngome ya kukabiliana na ushawishi wa nchi zinazotaka kuyatumia maslahi ya mataifa mengine kwa manufaa yao. Katika hotuba yake hiyo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha pia kama ninavyomnukuu:"Viongozi wa Marekani wanawaeleza viongozi wetu kwamba hawana nia ya kutaka kuubadilisha Mfumo wa utawala; wanasema uwongo, kwani kama wataweza hawatosita hata lahadha ndogo kufanya hivyo, lakini hawana uwezo kwa sababu Mfumo wa Kiislamu umeshikamana na imani, mapenzi na irada ya wananchi wote", mwisho wa kumnukuu. Kuhusiana na imani, mapenzi na irada hiyo ya wananchi, Ayatullah Khamenei amefafanua kama ninavyomnukuu tena:"Inshallah siku ya Bahman 22 (Februari 11) mtaona jinsi wananchi wa Iran watakavyojitokeza na kupaza sauti zao kuonyesha uimara, nguvu na uwezo wa taifa lao".
1372010

captcha