IQNA

Nasaha za Shahid Mutahhari kwa Ummah wa Kiislamu

12:24 - May 02, 2014
Habari ID: 1402070
Katika vipindi mbali mbali vya historia, wanafikra wameweza kunawiri katika nyuga za utamaduni na sayansi na hivyo kuwafungulia wanaadamu wengi njia ya nuru na saada.

Mitume wa Mwenyezi Mungu wakiongozwa na Mtume Muhammad SAW na  Ahlul Bayt wake watoharifu ndio walio katika daraja ya juu zaidi kwa mtazamo wa kuwaongoza wanaadamu.  Baada yao maulamaa na wanazuoni Waislamu ndio waliorithi jukumu la kueneza risala ya Mwenyezi Mungu. Shahid Murtadha Mutahhari ni moja kati ya nyota zilizong'ara katika ulimwengi wa elimu, amali njema , imani na akhlaqi bora. Aliweza kutia fora kwa kuingoza jamii iliyo katika kiza kuelekea katika nuru. Hatimaye wale walioshindwa kutoka katika kiza na kutostahamili nuru yake, hawakuwa na budi ila kumuua shahidi tarehe pili Mei mwaka 1979. Makala hii fupi itaangazia kwa muhtasari tu mfikra za mwanazuoni huyo maarufu kuhusu umuhimu wa kufuata njia sahihi katika kuunusuru Ummah wa Kiislamu..

Imam Khomeini MA, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran alisema hivi baada ya kuuawa shahidi Ustadh Mutahhari: "Mimi nimempoteza mtoto azizi sana ambaye ni natija ya umri wangu. Uislamu umepata pigo na pengo lisiloweza kuzibwa kwa kumpoteza huyo msomi ambaye athari zake zitadumu."

Imam Khomeini MA hakumsifu Shahid Mutahhari pasina kuwepo dalili. Kwa hakika Shahid Mutahhri alistahiki sifa kutokana na kuwa alibobea kikamilifu katika elimu na amali njema. Ameandika vitabu vingi kuhusu maudhui kama vile uadilifu wa Mwenyezi Mungu, utume, kukamilika utume, mwanaadamu kamili, sababu za kuelekea katika umaada, mfumo wa haki za mwanamke katika Uislamu na huduma mkabala na Iran na Uislamu.

Moja ya sifa za kipekee za Shahid Mutahhari ni kufahamu kwa umakini na undani masuala ya kijamii na mirengo mbali mbali ya kifikra hasa kuhusiana na vijana. Ustadhi huyu aliyebobea mbali na kubainisha kwa uwazi na kielimu fikra za Kiislamu, hali kadhalika alikuwa pia akitahadharisha sana kuhusu fikra potofu na kuzitaja kuwa chanzo cha kuzorota jamii ya Kiislamu. Ni kwa sababu hii ndio maana akatumia wakati wake mwingi kuielimisha jamii kuhusu fikra potofu na namna ya kuziepuka. Kwa kifupi ni kuwa ukiangazia vitabu na makala za Shahid Mutahhari utaona uso wa mwanamapambano dhidi ya ujinga na ujahili.

Tukiangazia aya za Qur'ani na riwaya tunaona kuwa kutafakari ni jambo ambalo limepewa umuhimu mkubwa katika Uislamu. Katika hadithi maarufu ya Mtume Muhammad SAW tunasoma kuwa : "Saa moja ya kutafakari ni bora kulika ibada ya miaka sabini."  Tab'aan riwaya hii haina maana kuwa thamani ya ibada iko chini au tupuuze ibada kwani kwa mujibu wa Qur'ani Tukufu sababu ya kuumbwa mwanaadmau ni kumuabudu Mola Muumba. Lengo la kauli hiyo ya Bwana Mtume ni kusisitiza kuhusu ulazima wa kufanya ibada inayoambatana na kutafakari na kufahamu kwa kina mafundisho ya dini. Hadithi hii pia inatufunza kuwa Uislamu ni dini ya elimu, fikra, uhakiki na mazungumzo. Tadaburi na tafakuri inaweza kuhusu aya za Qur'ani Tukufu, falsafa ya kuumbwa mwanaadamu, majina na sifa za Mwenyezi Mungu, riwaya na sunna za Mtume SAW na Ahul Bayt wake. Kwa msingi huo, ujinga, ujahili, kutojua, fikra kavu na zilizoganda pamoja na ria ni mambo ambayo yanakatazwa katika Uislamu.

Shahid Mutahhari aliuchukulia ujahili na fikra zilizoganda kuwa magonjwa mawili hatari kwa mwanaadamu na kuongeza kuwa hayo mawili hupelekea kudorora na kuzuia ustawi wa mwanaadmau na hatimaye kumuangamiza au kumpoteza. Aliamini kuwa ujahili humpelekea mtu kutamani mambo ya kidunia na kupotosha dini kwa kisingizio cha kuleta mabadiliko. Aidha aliamini kuwa ujahili hupelekea mwanaadamu kuwa na mgando wa kiakili na kutaja kila kitu kipya kuwa kilicho dhidi ya dini. Shahid Mutahhari aliamini kuwa msingi wa fikra finyu na taasubi zisizo na maana ni ujinga na ujahili. Iwapo nuru ya ujuzi na kutafakari itang'ara katika fikra za mwanaadamu, hakutakuwepo mahala pa mgando wa kifikra na ugumu wa kufahamu na hivyo dini itarejea mahala pake asili. Katika kubainisha hatari ya ujahili na mgando wa kifikra, Shahid Mutahhari alikumbusha kuhusu kisa cha kuibuka pote la Khawarij mwanzoni mwa Uislamu na kuandika: 'Katika vita vya Siffin wakati jeshi la Imam Ali AS lilikua linakaribia kuliangusha jeshi la Muawiyya, Amr ibn Aasambaye alikuwa kamanda wa jeshi la Muawiyya aliwaamuru wanajeshi wake wafunge Qur'ani katika ncha za mishale. Hapo kundi moja la askari wa Imam Ali AS kutokana na ujahili wao na mgando wa kifikra walihadaika na kuanza kutoa nara ya "لا حُکم اِلّا لِله" yaani hakuna hukumu ila ya Allah, na hatimaye wakaukataa uongozi wa Hadhrat Ali. Kimsingi ni kuwa waasi hao waliitafsiri kidhahiri sehemu ya aya ya 57 ya Surat al An'am isemayo 'hapana hukumu ila ya Mwenyezi Mungu.' Walifikiri kuwa jamii ya Kiislamu haihitaji kiongozi. Hii ni katika hali ambayo iwapo hatakuwepo  kiongozi, hukumu za Mwenyezi Mngu haziwezi kutekelezwa kikamilifu. Natija ya ujahili huu ni kuibuka kundi lenye misimamo mikali lililojulikana kama Khawarij ambalo lilidai kuwa wawakilishi wa sheria na warithi pekee wa Uislamu wa kweli na kudai kuwa wengine wote, akiwemo Imam Ali AS, hawakuufahamu  Uislamu. Walikuwa wakisema kuwa Mwislamu ambaye anatenda dhambi kubwa ametoka katika Uislamu na ni kafiri. Itikadi hii ilikuwa na taathira mbaya katika jamii ya Kiislamu. Watu hawa walijiona kuwa ndio wawakilishi pekee wa Uislamu na walimtuhumu kila Mwislamu ambaye hakuwa na nadharia sawa na yao kuwa kafiri na hivyo kujipa ruhusa ya kumwaga damu yake. Mfano wa suala hilo ni kisa cha Abdullah bin Khabab ambaye alikuwa sahaba wa Mtume SAW ambaye wakati alipokumbana na Khawarij na kuwaambia kuwa 'Ali bin Abi Talib anaijua  dini ya Allah zaidi yenu' walimuua kinyama pamoja na ndugu zake.

Msingi wa fikra za Khawarij ndio ule ule unaonekana katika fikra ambazo zimekuwa zikidhihiri kwa sura mbali mbali katika jamii za Kiislamu katika vipindi mbali mbali vya historia ya Uislamu. Shahid Mutahhari anasema: "Historia ya Khawarij ni ya kushangaza na yenye masomo na ibra kutokana na kile kinachojiri wakati itikadi ya kidini inapochanganyika na ujahili na taasubi kavu. Khawarij ni watu ambao walizama sana katika ibada kiasi cha kuonekana athari za ibada hizo ndefu katika mapaji ya nyuso na magoti yao. Aidha walikuwa tayari kutoa roho zao kwa ajili ya dini lakini kutokana na akili duni na sahali walikuwa na msimamo finyu sana na hivyo kuudhuru Uislamu kwa kiwango kikubwa. Waliibua unyama mkubwa kiasi kwamba, kwa kutamka tu maneno ya 'hakuna hukumu ila ya Allah' waliingiza hofu kubwa katika nyoyo za watu.

Katika kuthibitisha kuwa batili fikra za Khawarij, Ustadh Mutahhari alitumia maneneo ya Imam Ali AS kwa kusema: "Hadhrat Ali katika kupinga madai na itikadi za Khawarij alisema: "Mtume alikuwa akitoa hukumu ya kunyongwa mtenda jinai na baada ya hapo aliuswalia mwili huo Salatul Janaza. Kwa hivyo iwapo kufanya dhambi kubwa kunapelekea mtu kuwa kafiri Mtume hakupaswa kuisalia maiti hiyo kwani kwa mujibu wa Qur'ani Tukufu haijuzu kuiswalia maiti ya kafiri. Aidha alikuwa akimpiga viboko mlevi lakini hakuwa akikata au kumyima haki yake katika Baitul Mal."

Tukiangazia hali ya hivi sasa ya jamii ya Waislamu duniani tunaona kuwa tumefikiwa na hatari ambayo wanafikra kama Shahid Mutahhari walijaribu kuwaonya watu kuihusu na kwa hivyo kuna haja ya kuwepo mwamko. Kuibuka nadharia hatari ya kitakfiri ambayo kiitikadi na kivitendo inashabihiana sana na Khawarij wa zama za awali za Uislamu ni natija ya ujahili na mgando wa kifikra ambao unaonekana katika baadhi ya sehemu za jamii ya Kiislamu. Matakfiri, sawa na Makhawarij waliokuwa na fikra potofu, wanajiona kuwa ndio pekee wenye Uislamu halisi na huamua kumuua kinyama kila anayepingana nao. Imam Ali AS katika kubainisha sifa za Makhawarij na wale wote wenye fikra finyu na zenye mgando anasema: "Wao ni watu wenye kutumia mabavu wasio na fikra za hadhi ya juu na waliokosa hisia za ukarimu... Katika sehemu nyingine anawaambia: "Nyinyi ni wabaya zaidi miongoni mwa watu. Nyinyi ni mishale katika mkono wa shetani ambaye anawatumia kulenga shabaha na kwa kuwatumia, hutia shaka katika nyoyo za watu na kuwapotosha."

Moja ya hatari za watu wenye fikra kavu na zilizoganda ni kuwa hutia shaka nyoyo za watu wasio na busara na hivyo kuwafanya kushindwa kubainisha baina ya mrengo wa haki na batili. Shahid Mutahhari aliashiria namna fikra kama hizo zinavyopaswa kufichuliwa haraka kama ambavyo Imam Ali AS alivyokabiliana na Khawarij. Shahid Mutahhari anaongeza kwa kusema: "Moja ya maajabu ya historia ya maisha ya Ali AS ni namna alivyochukua hatua za kishujaa katika kupambana na waliojifanya kuwa watukufu ambao walikuwa na ghururi na fikra zenye mgando. Ali alitumia upanga wake dhidi yao na kuwafananisha na ugonjwa wa kichaa cha mbwa. Kama ambavyo wanyama huwa hawana uwezo wa kufikiri na hivyo huwashambulia wengine na kueneza ugonjwa huo, fikra hizo potofu nazo hatua kwa hatua huenea na kuichafua jamii ya Waislamu na kuuvunja Uislamu. Mtume Mtukufu SAW anasema: "Watu wawili wametuvunja, mjinga mwenye taasubu na msomi asiyejali."

Katika kipindi chote cha umri wake uliojaa baraka, Allamah Shahid Murtadha Mutahhari, alijitahidi sana katika kuondoa ufahamu potofu na ujahili katika uso wa Uislamu na hatimaye kutoa maisha yake mhanga akiwa katika njia hii ya Allah SWT. Ingawa imepita zaidi ya miongo mitatu tangu auawe shahidi lakini fikra zake zilizojaa nuru bado zingali zinaongoza nyoyo za watu wenye kutafuta haki.

1400836

captcha