Sheikh Ali Attiyah mwanazuoni mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Al Azhar amenukuliwa na kanali ya televisheni ya Al Alam akisema kuwa makundi ya magaidi Syria yanapata himaya ya Marekani na utawala haramu wa Israel. Ameongeza kuwa makundi hayo yanayodai kuwa ya Kiislamu yameanzishwa na Wazayuni na Marekani kwa lengo la kuwafarakanisha Waislamu na kuzisambaratisha nchi za Kiarabu. Naye Sayyid Faraj mmoja kati ya viongozi wa chama cha 'Ustawi na Maendeleo' Misri amelaani wanaowakufurusha Waislamu wenzao kwa sababu tu wanahitilafiana kimawazo. Mwanasiasa huyo wa Misri naye pia amesema anaamini kuwa Marekani na Israel ndio waungaji mkono wakuu wa magaidi wanaoendeleza vita dhidi ya Rais Assad wa Syria. Huku hayo yakijiri ripoti zinasema kuwa serikali ya Syria imefanikiwa kuwatimua kikamilifu magaidi wanaopata himaya ya kigeni ambao walikuwa wameuteka mji wa Homs. Machafuko Syria yalianza mwaka 2011 na serikali ya Damascus inazilaumu nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani, Uingereza na Ufaransa pamoja na waitifaki katika eneo yaani Saudi Arabia, Uturuki, Qatar na utawala wa Kizayuni wa Israel, kuwa ndio waungaji mkono wakuu wa magaidi wanaotaka kuiangusha serikali halali ya Rais Bashar Assad.