Mtandao wa habari wa al-Mayadeen umevitaja vyanzo hivyo vikisema kuwa ndege za kivita za utawala wa Israel zilishambulia makao makuu ya vita vya kielektroniki huko al-Bahdaliya, karibu na kaburi hilo takatifu Jumatatu jioni.
Hapo awali, kulikuwa na ripoti za milipuko mikubwa katika Wilaya ya Zeynabiya, ambapo mahala hapo patakatifu panapatikana.
Vyombo vya habari vya utawala ghasibu wa Israel vimetangaza kwamba jeshi la anga la utawala huo ghasibu limefanya mashambulizi 300 ya anga dhidi ya Syria katika muda wa siku mbili zilizopita na kuharibu miundombinu ya ulinzi na kijeshi ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa vyombo hivyo, ndege za kivita za utawala ghasibu wa Israel zimefanya makumi ya mashambulizi ya anga dhidi ya miundombinu ya ulinzi na kijeshi ya Syria jana usiku na asubuhi ya leo, jambo ambalo halijawahi kutokea mfano wake.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, utawala wa Kizayuni unatumia ombwe la utawala lililojitokeza baada ya kuanguka serikali ya Syria mikononi mwa wapinzani wenye silaha na kuporomoka mfumo wa ulinzi nchini Syria. Hadi hivi sasa utawala wa Kizayuni umeshalenga makumi ya makao makuu, vituo vya kisayansi, taasisi muhimu, viwanja vya ndege na mifumo ya ulinzi na rada ya nchi hiyo ya Kiarabu.
Televisheni ya Fox News ya Marekani imetangaza kwamba Israel imefanya mashambulizi 250 ya anga katika saa 48 zilizopita. Lakini vyombo vya habari vya utawala ghasibu wa Israel vimetangaza kuwa ndege za jeshi la anga la utawala huo dhalimu zimefanya mashambulizi 300 dhidi ya Syria katika muda wa siku mbili zilizopita.
Televisheni ya Al-Mayadeen ya Lebanon pia imenukuu duru yake ya ndani na kusema kwamba, jeshi la Israel llmeendelea na uvamizi wake wa nchi kavu ndani ya ardhi ya Syria na kwamba vifaru vyake vimekaribia mji mkuu wa Syria, Damascus.
Hujuma dhidi ya Golan
Kwingineko, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) imelaani "vitendo haramu" vya utawala wa Kizayuni wa Israel nchini Syria, ambapo utawala huo ghasibu unatumia fursa ya hali ya machafuko kupanua ukaliaji wake wa mabavu wa ardhi ya nchi hiyo ya Kiarabu.
Jumuiya hiyo yenye wanachama 22 imetoa taarifa kulaani hatua haramu za Israel ikisema kuwa ni: "pamoja na majaribio ya kupanua uvamizi katika Miinuko ya Golan au kubatilisha kwa upande mmoja mkataba wa 1974, hatua ambazo zinakiuka waziwazi sheria za kimataifa."
Kauli hiyo imekuja saa chache baada ya wanamgambo wanaoungwa mkono na mataifa ya kigeni, wakiongozwa na Hay’at Tahrir al-Sham (HTS), kuuteka mji mkuu wa Syria, Damascus, na kutangaza kuanguka kwa serikali ya Rais Bashar al-Assad.
Muda mfupi baadaye, jeshi la utawala Israel liliteka eneo linalotenganisha Miinuko ya Golan ya Syria inayokaliwa kwa mabavu na utawala huo na maeneo mengine ya Syria, pamoja na miji miwili ya Mkoa wa Quneitra.
Wanajeshi wa Israel sasa wanaelekea maeneo ya Dara’a, yaliyoko takriban kilomita 90 (maili 56) kusini mwa mji mkuu Damascus.
Waziri Mkuu wa utawala huo, Benjamin Netanyahu, alisema siku ya Jumapili kwamba makubaliano ya miongo kadhaa na Syria yamesambaratika, na kwa msingi huo amemuru vikosi vya Israel kunyakua eneo la kando ya Milima ya Golan baada ya wanajeshi wa Syria kujiondoa punde baada ya serikali ya Assad kuanguka.
Jeshi la Israel pia lilitoa onyo, likiwataka wakaazi wa miji mitano ya kusini mwa Syria kusalia majumbani mwao hadi taarifa nyingine kwani lilifanya mashambulizi kadhaa ya anga dhidi ya vituo vya kijeshi vya Syria. Miji hii ni Ofania, Quneitra, al-Hamidiyah, al-Samadaniyah ya magharibi, na al-Qahtaniyah.
3491000