Rais Rouhani ameyasema hayo leo mjini Tehran katika kongamano la kimataifa la ‘Siku ya Msikiti Duniani’ ambapo amekumbusha kuhusu kibla cha kwanza cha Waislamu yaani Msikiti wa Al Aqsa ambao hivi sasa unakaliwa kwa mabavu na utawala vamizi na katili wa Israel. Amesema Msikiti wa Al Aqsa ni msikiti ambao ulitumiwa na manabii wengi wakubwa kwa ajili ya ibada. Rais wa Iran amesisitiza kuwa, ulimwengu wa Kiislamu na Waislamu hasa Maulamaa wa Kiislamu hawatakubali kuona kibla cha kwanza cha Waislamu kikibaki katika makucha ya maghasibu na wavamizi.
Kwingineko katika hotuba yake Rais Rouhani amesema ‘Siku ya Kimataifa ya Msikiti’ ni kielelezo kuwa msikiti ungali kituo cha kuwaogoza watu katika kuanzisha harakati na mapinduzi ambayo ni kwa maslahi ya umma.
Rais wa Iran amesema msikiti ulikuwa na nafasi kubwa katika mapinduzi na harakati ya Kiislamu ambapo kwa uongozi wa Imam Khomeini MA, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalipata ushindi.
Rais Rouhani amesema serikali yake inanufaika na nasaha za wanazuoni, maulamaa na wanafikra wa Kiislamu. Ameongeza kuwa wanazuoni wa kidini wana jukumu zito la kufikisha ujumbe wa Uislamu kote duniani. Amesema Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yamefanikiwa kukabiliana na njama za maadui kutokana na matumaini ambayo wanazuoni wameweza kuleta katika nyoyo za wananchi.