IQNA

Iran haitashirikiana na Marekani katika kadhia ya Daesh

20:07 - September 15, 2014
Habari ID: 1450408
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei asubuhi ya leo ameruhusiwa kuondoka katika Hospitali ya Shahid Rajai mjini Tehran baada ya kukamilisha matibabu na kupata nafuu kikamilifu.

Kabla ya kuondoka hospitali hapo, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alifanyiwa mahojiano na mwandishi habari wa Shirika la Matangazo la Iran (IRIB) akieleza kuridhishwa na upasuaji na matibabu aliyopewa na akasema: “Ninarejea nyumbani nikiwa mzima wa afya ya mwili na mwenye nishati. Ninawashukuru wananchi kwa upendo wao walionionesha katika siku kadhaa zilizopita na ninaona haya na kujihisi mwenye deni zito kwa wananchi.”

Ayatullah Khamenei ameshukuru matabaka yote ya wananchi, viongozi wa kidini, shakhsia mbalimbali, wakurugenzi, wanasiasa, wasanii na wanamichezo kwa upendo wao mkubwa na kusema kuwa mbali na upendo huo wa wananchi wa Iran, mataifa mengine pia yameonesha upendo mkubwa kwake. Amesema suala hili limetilia mkazo sisitizo lake la siku zote kwamba taifa la Iran lina nafasi ya kistratijia baina ya mataifa mengine.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema hakuna mfumo na nchi nyingine yenye mfungamano mkubwa wa kiroho, kiitikadi na kiimani kama huo na mataifa mengine nje ya mipaka yake.

Vilevile ameshukuru timu ya madaktari na wauguzi wa hospitali alipokuwa amelazwa na kusema kuwa: “Mtu anayejua uwezo mkubwa wa kielimu na umahiri wa matabibu na wauguzi wa hapa nchini anaona fahari kwa kuwa na utajiri huo mkubwa wa kibinadamu katika sekta ya afya ambayo ni miongoni mwa sekta muhimu sana za maisha ya wananchi na jamii.

Katika sehemu nyingine ya mahojiano yake Ayatullah Khamenei amesema: “Katika siku kadhaa nilizokuwa nimelazwa hapa hospitalini nimepata burudani ya kusikiliza matamshi ya viongozi wa Marekani kuhusu mapambano dhidi ya kundi la Daesh; hakika matamshi hayo yalikuwa kichekesho.”

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa matamshi yaliyotolewa na viongozi wa Marekani kuhusu suala la kupambana na kundi la Daesh ni upuuzi mtupu na yenye mwelekeo maalumu. Ameashiria matamshi yaliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani na msemaji wa wizara hiyo ambao wamesema waziwazi kuwa Iran haitaalikwa kushiriki katika mapambano dhidi ya kundi la Daesh na kusema: “Suala kwamba Marekani imekataa tamaa kwa kushiriki Iran katika kazi iliyo kinyume cha sheria ambayo pia si sahihi ni fakhari kwetu sisi, na hatujui fakhari kubwa zaidi ya hii”.

Baada ya hapo Ayatullah Khamenei ameweka wazi uongo wa Wamarekani katika madai yao ya kupambana na kundi la Daesh.

Amesema katika siku ngumu za mwanzoni mwa mashambulizi ya Daesh huko Iraq, balozi wa Marekani nchini humo alimuomba balozi wa Iran mjini Baghdad kwamba Iran na Marekani zifanye kikao kwa ajili ya mazungumzo na kupanga mikakati kuhusu kundi la Daesh.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: “Balozi wetu nchini Iraq aliakisi suala hilo hapa nchini na baadhi ya viongozi hawakupinga fikra ya kufanyika kikao hicho, hata hivyo mimi nilipinga na kusema, hatutashirikiana na Marekani katika kadhia hii kwa sababu wana nia mbaya na wameshirikiana na Daesh. Kwa msingi huo tunaweza vipi kushirikiana na Wamarekani katika hali kama hiyo?”

Ayatullah Ali Khamenei ameashiria matamshi yaliyotolewa siku chache zilizopita na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani akitangaza kuwa Washington haitaialika Iran katika muungano wa kupambana na Daesh, na kusema kuwa, Waziri huyo huyo wa Mambo ya Nje wa Marekani mwenyewe alimuomba Dakta Zarif (Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran) kwamba Iran ishirikiane na Marekani katika kadhia ya Daesh lakini Dakta Zarif akakataa.

Ameongeza kuwa, hata Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ambaye ni mwanamke na watu wote wanamjua, alikariri ombi hilo katika mazungumzo yake na Bwana Araqchi (Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran) lakini pia Araqchi amekataa ombi lake.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria upinzani wa wazi wa Jamhuri ya Kiislamu dhidi ya kushirikiana na Marekani katika kadhia ya kupambana na kundi la Daesh na akasema kuwa, Wamarekani wanaongopa kwamba hawataishirkisha Iran katika muungano wa kukabiliana na Daesh, wakati Iran ndiyo iliyokataa kushiriki katika muungano huo tangu hapo mwanzoni.

Ayatullah Khamenei amesema: “Hapo kabla na kwa makelele mengi, Wamarekani walianzisha muungano dhidi ya Syria kwa kuzishirikisha nchi nyingi lakini hawakuweza kufanya lolote; na huko Iraq pia mambo yatakuwa hivyo hivyo.

Amesisitiza kuwa Wamarekani hawana nia ya kweli ya kuchukua hatua kali dhidi ya kundi la Daesh na kuongeza kuwa, Wamarekani wenyewe wanaelewa vyema kwamba harakati iliyovunja mgongo wa Daesh huko Iraq si Marekani, bali ni wananchi na jeshi la Iraq ambao walijua vyema jinsi kupambana na Daesh na kutoa pigo kali kwa kundi hilo.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa kipigo cha wananchi na jeshi la Iraq dhidi ya Daesh kitaendelea na kuongeza kuwa, ukweli ni kuwa Wamarekani wanatafuta kisingizio cha kuwawezesha kufanya yale wanayoyafanya nchini Pakistan huko Iraq na Syria, kwani licha ya kuwapo serikali na jeshi imara, wanaingia katika ardhi ya nchi hiyo bila ruhusa na kupiga mabomu katika maeneo mbalimbali.

Amesema kuwa Wamarekani wanapaswa kuelewa kwamba, iwapo watafanya hivyo watakumbana tena na matatizo kama yale waliyokutana nayo nchini Iraq katika kipindi cha miaka kumi.

Mwishoni mwa mahojiano yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kwa vyovyote vile katika siku kadhaa zilizopita, matamshi ya viongozi wa Marekani yalikuwa burudani katika kitanda cha hospitali.

Kabla ya kuondoka hospitalini hapo pia Ayatullah Ali Khamenei amemtembelea na kumjulia hali Ayatullah Mahdavi Kanii ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu.

1450182

Kishikizo: khamenei daesh hospitali
captcha