Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliongoza umati mkubwa wa waumini kwenye sala ya maiti, iliyofanyika katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Tehran mapema asubuhi. Taarifa zinasema kuwa, viongozi wote wa ngazi za juu nchini akiwemo Rais, Spika wa Bunge, Mkuu wa Mahakama pamoja na wajumbe wa baraza la wanazuoni wataalamu wanaomchagua Kiongozi Muadhamu, wabunge, mawaziri, viongozi wa ngazi za juu wa kijeshi na matabaka mbalimbali ya wananchi wameshiriki kwenye sala hiyo ya maiti. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu licha ya kuongoza sala ya maiti ya Ayatullah Mahdavi Kani, alisoma Fatiha na kumuombea maghfira kwa Mwenyezi Mungu SW. Inafaa kuashiria hapa kuwa, Ayatullah Mahdavi Kani alifariki dunia hospitalini siku ya Jumanne iliyopita akiwa na umri wa miaka 81, baada ya kupatwa na matatizo ya moyo wakati aliposhiriki kwenye kumbukumbu ya kutimia miaka 25 ya kufariki dunia Imam Khomeini MA tarehe 4 Juni mwaka huu.../mh