Papa Benedict wa XVI ameyasema hayo mwishoni mwa kikao cha kimataifa kilichowajumuisha pamoja wanafikra wa Kiislamu na Kikristo mjini Vatican. Shirika la habari la Qurani la Kimataifa (IQNA) limeandika kwamba Papa Benedict amewataka viongozi wa kisiasa na kidini kufanya juhudi za kudhamini uhuru wa kuchagua itikadi na kuabudu kote duniani. Amesema, ana matarajio kwamba, haki ya kimsi za binadamu zitalindwa na watu wote. Kiongozi wa Wakatoliki Duniani amesema, kikao cha kimataifa cha wanafikra wa Kiislamu na Kikristo kilichofanyika Vatican ni hatua kubwa ya kuelekea kwenye maelewano na kufahamiana kati ya viongozi wa dini mbili za Kiislamu na Kikristo. Amesema kuwa hii leo watu wa dini wanabaguliwa na kutendewa ukatili mkubwa katika maeneo mbalimbali duniani na kwamba inasikitisha kuwa ubaguzi na ukatili huo unafanyika kwa kutumia jina la dini. Amewataka Waislamu na Wakristo kushirikiana na kuheshimiana kwa shabaha ya kulinda utukufu na haki za kimsingi za mwanadamu. Amesisitiza kwamba ni kwa kuheshimiwa utukufu wa mwanadamu tu ndipo mazingira yanayofaa yanaweza kuandaliwa kwa ajili ya wanadamu wote kuishi duniani kwa amani licha ya kuwa na tofauti za rangi na lugha. Amesema, viongozi wa kisiasa na kidini wanapasa kuheshimu haki za kila mtu na kumdhaminia uhuru wake wa kujieleza na kuabudu.
Kikao cha kimataifa cha Wanafikra wa Kiislamu na Kikristo kilimalizika alkhamisi ya wiki hii kwa kutolewa taarifa ya pamoja ambayo imesisitiza juu ya kufunguliwa mlango wa mazungumzo kati ya Uislamu na Ukristo, kuheshimu hadhi na utukufu wa mwanadamu, wito wa udugu na urafiki kwa msingi wa imani ya Mwenyezi Mungu Mmoja, udharura wa kutafuta njia bora za kutambua na kuondoa hali ya ukosefu wa maelewano kati ya wafuasi wa dini za Uislamu na Ukristo na udharura wa Waislamu na Wakristo kutambua misingi ya mafunzo ya dini za mbinguni.
Kikao hicho cha Vatican kimefanyika kufuatia ombi lililotolewa na wasomi 137 wa Kiislamu, baada ya matamshi ya dharau na kejeli yaliyotolewa na Papa Benedict dhidi ya Uislamu akiwa safarini nchini Ujerumani. 316855