IQNA

Nasrullah asisitiza kushindwa kwa siasa za Marekani Mashariki ya Kati

13:39 - November 12, 2008
Habari ID: 1707514
Sayyid Hassan Nusrullah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Lebanon amesisitiza kushindwa kwa siasa za Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati na hasa katika nchi za Iraq na Afghanistan.
Akizungumza jana Jumanne kwa mnasaba wa kuhuishwa kumbukumbu ya Shahid Ahmad Qaswir, mwanamapambano wa kwanza wa Lebanon kuuawa shihidi, na vilevile kuwadia Siku ya Shihidi, Sayyid Hassan Nusrullah amesema kuwa chanzo halisi cha kufeli siasa za Marekani ulimwenguni ni mapambano yanayoonyeshwa na mataifa mbalimbali dhidi ya njama za nchi hiyo. Amesema kuwa harakati ya Hizbullah hivi sasa iko katika hali nzuri zaidi kijeshi kuliko wakati mwingine wowote ule na kwamba, utawala ghasibu wa Israel utakabiliwa na pigo kubwa la kijeshi na la kufedhehesha iwapo utafikiria tena kutaka kuivamia Lebanon kwa madhumuni ya kutaka kuikandamiza harakati hiyo. Huku akisisitiza umuhimu wa kuimarishwa kijeshi jeshi la Lebanon kwa lengo la kukabiliana na uchokozi wa utawala haramu wa Israel, Sayyid Nasrullah amesisitiza kwamba Hizbullah daima iko katika hali ya kujiimarisha kijeshi kwa lengo la kukabiliana na uchokozi wowote wa Wazayuni. Amesema, utawala huo daima unafanya ujasusi katika ardhi ya Lebanon na kuogeza kuwa, kufichuliwa kwa shughuli za kijasusi za utawala huo katika ardhi ya Lebanon ni mafanikio makubwa kwa jeshi la nchi hiyo. Nasrullah pia amesema kuwa Hizbullah inaunga mkono juhudi zozote za usalama zitakazofanyika kati ya Lebanon na Syria kwa shabaha ya kudhamini maslahi ya nchi hizo. Mwishoni amezitaka nchi zote za Kiislamu na Kiarabu kupinga kushiriki kwa watawala wa Kizayuni katika kikao cha mazungumzo ya kidini kinachotazamiwa kufanyika hivi karibuni mjini New York Marekani. 318940

captcha