Kwa mujibu wa gazeti la ar-Rai la nchi hiyo, kikao hicho cha siku tatu kimeandaliwa na Kamati ya Kimataifa ya Mielekeo ya Wastani, chini ya anwani 'kuelekea kuufahamu Uislamu.' Idadi kubwa ya wanazuoni, wanafikra, wahubiri, na shakhsia wa kisiasa wa nchi za Kiislamu na Kiarabu wanashiriki katika kikao hicho.
Marwan al-Fauri mkuu wa kamati iliyotajwa amesema duru ya nne ya kikao hicho inafanyika katika hali ambayo, ulimwengu unashuhudia mabadiliko yanayoenda kwa kasi kubwa na kwamba wanafikra wa Kiislamu wanapasa kutoa mitazamo na kutafuta njia bora za ufumbuzi wa matatizo ya ulimwengu wa Kiislamu, zinazokwenda sambamba na utamaduni wa ulimwengu wa leo. Amesema, lengo hasa la kuandaliwa kikao hicho ni kukabiliana na changamoto zilizopo, kutatua matatizo na changamoto za ndani na nje ya ulimwengu wa Kiislamu, kuwasilisha sura halisi ya Uislamu kwa wasiokuwa Waislamu, kukabiliana na hujuma ya kidhulma ya nchi za Magharibi dhidi ya Uislamu, kuunga mkono sira na sunna za Mtume Mtukufu (saw) na vilevile kulinda ujumbe wake wa kudumu milele. Al-Fauri amesisitiza kwamba, kuimarisha umoja wa Waislamu ulimwenguni, kuzuia kutawanyika kwao na fitina miongoni mwa wafuasi wa madhehebu mbalimbali za Kiislamu, kuepuka taasubi, kuimarisha nafasi ya Waislamu katika mkondo wa ustawi wa jamii ya mwanadamu na kuwashirikisha katika maendeleo ya ulimwengu wa leo ni malengo mengine ya kikao hicho. Amesema, mambo mengine yatakayojadiliwa katika kikao hicho cha Amman ni pamoja na kuimarishwa kwa uhusiano wa nchi za Kiislamu na Kiarabu, kuenezwa ujumbe wa kibinadamu na Uislamu wa misimamo ya kati kwa kati, kuwafahamisha watu wasiokuwa Waislamu mafundisho ya Kiislamu, kushajiisha usamehevu, kushajiisha mazungumzo na kujitenga na misimamo mikali na ya utumiaji nguvu, kuimarisha mazungumzo ya tamaduni na ustaarabu tofauti na kuimarisha nafasi ya mwanamke katika maendeleo ya jamii ya Kiislamu. Mwishoni al-Fauri amesema kuwa shughuli za kamati hiyo zimepokelwa na kuungwa mkono na nchi nyingi za Kiarabu na Kiislamu. 320937