Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA katika eneo la Balkan, meya huyo aliamuru msikiti huo uharibiwe katika siku ya mwisho ya sherehe za idul-Adh'ha. Msikiti ulio katika mtaa wa Meden tayari umeshaharibiwa.
Meya huyo ambaye alichaguliwa kwa tiketi ya chama kipya cha GERB ametuhumiwa mara kadhaa kwa kuwa na misimamo ya kibaguzi.
Baada ya kuharibiwa msikiti huo Chama cha Waislamu wa Kituruki Bulgaria MRF ambacho ni kati ya vyama muhimu katika serikali ya mseto nchini humo kimetoa taarifa na kulaani vikali kitendo cha meya huyo mbaguzi. Mbunge wa chama hicho Nasrin Uzun amezunguma katika kikao cha bunge la kitaifa na kusoma tamko la chama chake kuhusu kuharibiwa msikiti katika mtaa wa makaazi wa Meden Rudnik. Amesema, siku moja tu baada ya kuadhimishwa mwaka wa 60 tangu kuidhinishwa Mkataba wa Kimataafa wa Haki za Binaadamu na siku ya mwisho ya sherehe za Idul-Adh'ha, Meya wa Burgas aliamuru msikiti wa Waislamu kubomolewa katika mji huo wa pwani.
Mji wa Burgas ulio katika Bahari Nyeusi ni kati ya miji muhimu ya Bulgaria. Chama kipya cha GERB kina ushawishi mkubwa mjini humo. Kuna Waislamu zaidi milioni moja nchini Bulgaria au asilimia 14 ya raia wote wa nchi hiyo.
Waislamu nchini Bulgaria walianza kukandamizwa na kuuawa kwa umati wakati wa Vita vya Msalaba na wakati wa watawala wa Kikomunisti. Hata baada ya kusambaratika Ukomunisti, Waislamu wa Bulgaria, sawa na wenzao katika eneo la Balkan, wamekuwa wakikandamizwa, kudhalilishwa na kubaguliwa. Pamoja na hayo kutokana na kumtegemea Mwenyezi Mungu, imani thabiti na subira ya Waislamu wa Bulgaria, Uislamu unaendelea kukua barani Ulaya na kuleta mabadiliko ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.
335555