Amesema Waislamu wa Kishia sambamba na kulinda na kutetea itikadi yao iliyowazi na yenye ushahidi madhubuti ya tukio la Ghadir, kamwe hawataruhusu itikadi yao hiyo iwe chanzo cha hitilafu na mifarakano katika ulimwengu wa Kiislamu.
Ayatullah Khamenei aidha ametoa mkono wa baraka ya Idi tukufu ya Ghadir kwa taifa muumini la Iran na mataifa mengine yote ya Waislamu, na amesema kwamba, kuwa na maarifa sahihi kuhusu tukio la Ghadir hufanya harakati ya umma wa Kiislamu kwenda njia iliyo sawa na kwamba hatua muhimu sana aliyochukua Mtume Muhammad SAW ya kuainisha mtu wa kushika nafasi yake yaani Amirul Muuminin Ali bin Abi Talib AS tena mwishoni mwa maisha yake Bwana Mtume yaliyojaa baraka, kwa kweli ni hatua inayoonyesha umuhimu wa kuwa na serikali na mshikamano uliopo baina ya dini na siasa katika Uislamu. Amesisitiza kuwa, umma mzima wa Kiislamu leo hii unapaswa kupata funzo kubwa katika tukio hilo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran pia amesema kubainisha na kuweka wazi kigezo cha serikali ya Kiislamu ni somo jingine lililomo katika tukio adhimu la Ghadir na kuongeza kuwa, kutangazwa mtu mtukufu kama Imam Ali bin Abi Talib AS kuwa mtu wa kushika nafasi ya Bwana Mtume Muhammad SAW kunaonyesha kuwa Ghadir si kumbukumbu ya kihistoria tu kwa Waislamu, bali tukio hilo linaweka wazi vigezo vya kufuatwa katika kuongoza jamii za Kiislamu na jamii zote za mwanaadamu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema miongoni mwa sifa maalumu za Imam Ali AS zilikuwa ni wakati wote kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu, kufanya jitihada kubwa na bila kuchoka katika njia ya Mwenyezi Mungu, kujitolea mhanga katika njia ya haki na ukweli, subira na istikama madhubuti kama chuma cha pua katika kukabiliana na maadui wa Mwenyezi Mungu, kutojali mapambo ya dunia na kuwajali na kuwatumikia wanaadamu dhaifu na madhulumu na ameongeza kuwa, tukio la Ghadir linaufunza umma wa Kiislamu kwamba uongozi wa jamii za Kiislamu unapaswa kuwa mikononi mwa watu ambao wanamfanya Imam Ali kuwa ni kigezo na nembo yao na ambao wanafanya juhudi za kukikaribia kilele hicho adhimu. Amesema, jambo hilo muhimu ni miongoni mwa ujumbe mpya wa Uislamu uliojaa utukufu ambao Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inautoa kwa walimwengu leo hii.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile amesema, Ali bin Abi Talib AS alikuwa ni mwanafunzi mkubwa wa Mtume Mtukufu SAW katika subira, jitihada na sifa nyinginezo na kuongeza kuwa, umaskini mkubwa ilio nao jamii ya mwanaadamu leo hii ni kukosa wanasiasa wenye sifa bora ambao Uislamu umeonyesha mfano wake katika tukio la Ghadir Khum.
Vile vile ameashiria kuweko mitazamo na ufahamu tofauti wa tukio la Ghadir kati ya Waislamu wa Kishia na Kisuni na kusisitiza kwamba, pamoja na kuweko tofauti hizo za mitazamo, lakini Mashia na Masuni wote wanakubaliana kuhusu asili ya tukio la Ghadir na utukufu wa Imam Ali AS na kwamba Waislamu wote duniani, wanaamini kuwa Ali bin Abi Talib AS ni nukta ya juu na kilele kisichofikika katika upande wa elimu, takwa na ushujaa.
Ayatulah Khamenei aidha amesisitiza juu ya haja ya kuwa macho kikamilifu Waislamu wa Kishia na Kisuni katika kupambana na njama za kuleta mifarakano baina yao na kuongeza kwamba, kuwa na imani thabiti ya Uimam wa Amirul Muuminin Ali bin Abi Talib AS baada ya Mtume Muhammad SAW ndio msingi mkuu wa itikadi ya Kishia na Waislamu wa madhehebu hayo na kwamba Waislamu hao wamedumisha na wataendelea kudumisha itikadi hiyo na maarifa na elimu nyingine bora licha ya kuweko dhulma kubwa na uadui mkubwa dhidi yao, lakini pamoja na hayo, kamwe hawataruhusu itikadi hiyo iwe chanzo cha hitilafu na mizozo katika ulimwengu wa Kiislamu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia bidii zisizochoka za Imam Khomeini MA na Jamhuri ya Kiislamu kwa ajili ya kuzuia kuzuka hitilafu miongoni mwa Waislamu na ameongeza kuwa, mabeberu wa dunia ambao wamepata pigo kutokana na mshikamano na kukurubiana nyoyo za mataifa ya Kiislamu wawe Mashia au Masuni, hivi sasa wanaona njia bora kabisa ya kuleta mizozo, mifarakano na ugomvi kati ya Waislamu na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuzusha na kukuza taasubu na chuki za kimadhehebu, na inabidi kuwa macho kikamilifu mbele ya njama hizo hatari sana.
Ayatullah Udhma Khameni ameashiria pia kuwekeza maadui wa umma wa Kiislamu kwenye suala la kuleta mifarakano na kukumbusha kuwa, tangu huko nyuma hadi leo hii tunajua kwamba pesa za kuchapishia vitabu vilivyo jaa chuki na matusi dhidi ya Waislamu wa Kishia na Kisuni zinatolewa na taasisi moja yenye mfungamano na ubeberu na je tukio hilo la hatari sana je, si onyo la kuwaamsha waliolala?
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema kuchapishwa vitabu vya kutukana Mashia au Masuni katika ulimwengu wa Kishia na Kisuni kunasaidia na kuhudumia malengo ya Marekani na Uzayuni na amesisitiza kuwa, kila mmoja ajue kwamba vitabu vya aina hiyo haviwezi kumfanya Mshia yeyote kuwa Msuni na wala havivutii moyo wa Msuni yoyote kuwa Mshia.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa mwisho wa kushikamana na kuomba msaada kupitia kumkubali na kumfuata Imam Ali AS na kusisitiza kuwa, hakuna tatizo lolote kusambaza vitabu vyenye ushahidi madhubuti na wa kimantiki, kama ambavyo maulamaa wa Kishia wamekuwa wakifanya katika kipindi chote cha historia na bila ya shaka wataendelea kufanya hivyo, lakini kama mtu atadhani kuwa akiwapaka matope na kuwatukana Waislamu wa Kisuni atakuwa ndio analinda itikadi za Kishia ajue kwamba hakuna faida yoyote anayoipata zaidi ya kuongeza moto wa chuki na kwa kweli kitendo chake hicho si cha kulinda itikadi ya wilaya bali ni kuitia nguvu na kuilinda Marekani na Wazayuni.
Vile vile ameashiria njama za watu baki za kujaribu kuwashawishi viongozi wa baadhi ya nchi za Kiarabu kupambana na haki ya nyuklia na malengo mengine ya taifa la Iran na kuongeza kuwa, hilo ndilo kubwa lililobakia analoweza kulifanya adui na fauka ya hayo ni kuwa serikali hizo nazo zinazingatia kazi zao na haziko tayari kuona zimedhibitiwa kikamilifu na Marekani na Wazayuni kwa kisingizio cha suala la kukabiliana na Iran.
Mwishoni mwa hotuba yake Ayatullah Khemenei amesisitiza kuwa, iwapo taifa la Iran na mataifa mengine ya Kiislamu yatakuwa macho, njama zozote za mabeberu hazitaweza kamwe kufanikisha malengo yao ya chuki ya kutaka kuudhoofisha uma wa Kiislamu.
Mwanzoni mwa mkutano huo, msoma mashairi mmoja wa mashairi ya Ahlul Bayt As, amepata fursa ya kusoma mashairi kuhusu Imam Ali AS na tukio lililojaa baraka la Ghadir.