Kwa mujibu wa gazeti la al Mustaqbal la Beirut, Fuad Siniora Waziri Mkuu wa Lebanon alitoa tangazo akisema kuwa Walebanon wataomboleza na kutafakari mkasa wa Gaza. Amesema, lengo kuu ni kuonyesha ufungamano na watu wa Palestina na hasa familia za mashahidi wa Gaza. Kwa kuzingatia hayo bendera za Lebanon zilipepea nusu mlingoti Jumatano ya jana katika idara na mashirika ya serikali. Aidha vituo vya radio na televisheni nchini humo vilitakiwa kusitisha matangazo ya kawaida na badala yake kutangaza matukio na vipindi vinavyohusiana na maafa ya kusikitisha huko Gaza.
Wakati huo huo Rais Michel Suleiman wa Lebanon ametangaza kuwa Beirut iko tayari kuandaa kikao cha viongozi wa nchi za Kiarabu iwapo kutaendelea kuwepo hitilafu kuhusu ni wapi mkutano huo ufanyike.
Kwa mujibu wa mtandao wa intaneti wa Elnashra, Suleiman amesema, kikao cha dharura cha viongozi wa nchi za Kiarabu kinatakiwa kufanyika Damascus kwa vile Syria ndiye Mwenyekiti wa kiduru wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu. Hata hivyo kutokana na kuwa kikao cha mwisho cha jumuiya hiyo kilichofanyika Damascus mwezi Machi 2008 kilisusiwa na nchi kadhaa za Kiarabu, kuna uwezekano kitendo hicho kikarudiwa tena. Suleiman amesisitiza tena wito wake wa kufanyika kikao cha dharura cha viongozi wa nchi za Kiarabu ili kuchukua msimamo wa pamoja wa Kiarabu kuhusu jinai za Wazayuni huko Gaza.
341668