Jordan imemwita nyumbani balozi wake anayehudumu huko Tel Aviv katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel. Kwa mujibu wa ripoti zinazotolewa kuhusiana na suala hilo, watawala wa Jordan wameshurutisha kurejea kwa balozi huyo mjini Tel Aviv na kusimamishwa mashambulio ya kinyama ya Wazayuni katika Ukanda wa Gaza.
Gazeti la utawala haramu wa Israel la Yediot Ahronot pia limesema kuwa, Jordan imechukua hatua ya kumwita nyumbani balozi wake kutoka Tel Aviv kama alama ya kulalamikia mashambulio yake dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza. Jordan imelazimika kuchukua hatua hiyo isiyo na uzito mkubwa baada ya wananchi wa nchi hiyo kufanya maandamano makubwa dhidi ya siasa za nchi hiyo kuhusiana na utawala haramu wa Israel unaoendelea kuwachinja kinyama ndugu zao wasio na hatia katika Ukanda wa Gaza.
Maandamano yaliyofanywa Ijumaa na wananchi hao karibu na ubalozi wa utawala haramu wa Israel huko Amman yalipelekea kuzuka mapigano kati yao na polisi ya nchi hiyo waliowazuia kuelekea katika ubalozi huo ili kubainisha malalamiko yao dhidi ya Wazayuni.
Wajordan wamekuwa wakifanya maandamano ya mara kwa mara wakilaani vikali jinai zinazotekelezwa na utawala haramu wa Israel dhidi ya wakazi wasio na ulinzi wa Ukanda wa Gaza na kutaka balozi wa utawala huo afukuzwe nchini humo. 345695