Ni karibu miaka 12 sasa ambapo Israel, ikisaidiwa na Marekani na baadhi ya jamii za Magharibi wamekuwa wakiwaua, kuwatia nguvuni na kuwatesa wanachama wa harakati ya Hamas na vilevile kuwawekea vikwao na mzingiro, lakini nguvu na uungaji mkono wa watu kwa harakati hiyo unaongezeka siku baada ya siku.
Hayo amesemwa na mwandishi wa Kimarekani Patrick Martin katika makala iliyopewa kichwa cha habari "Hamas Kamwe Haitakufa". Patrick Martin ameandika kuwa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas kamwe haitaitambua rasmi Israel, kwani hatua hiyo ni sawa na kukubali uvamizi na kusalimu amri mbele ya jinai za kivita za Israel.
Mwandishi huyo Mmarekani ameandika kuwa: Kufuatia kushadidi mashambulizi ya kinyama ya Israel katika Ukanda wa Gaza wanachama wa Hamas wamerejea kwenye mbinu yao ya zamani ya kijeshi ya kutekeleza operesheni za kujitolea mhanga na kufa shahidi.
Patrick Martin ameandika katika makala hiyo kwamba: Mashambulizi ya nchi kavu ya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza na kuongezeka idadi ya watu waliouawa na kujeruhiwa hakujadhoofisha azma ya mapambano ya wanachama wa harakati ya Hamas na wananchi wa Gaza bali nguvu za kijeshi za harakati hiyo zimeongezeka.
Mwishoni mwa makala yake, mwandishi huyo wa Kimarekani anasema: Wakati wimbi la makombora linazidi kumiminika Ukanda wa Gaza, kundi la madaktari wa Kiarabu limevuka mpaka wa Misri, nchi inayoshirikiana na Israel katika kutenda jinai dhidi ya Wapalestina, na kuingia Gaza kwa ajili ya kusaidia wagonjwa na majeruhi wa mashambulizi ya Israel, suala ambalo linaweka wazi umashuhuri na uungaji mkono wa umma wa Kiarabu na Kiislamu kwa harakati ya Hamas. 345940