Mjadala huo ulihudhuriwa na shakhsia wa kielimu, kiutamaduni na kidini kama Mufti Muhammad Mukarram Ahmad ambaye ni Imamu wa msikiti wa Ijumaa wa New Delhi, Maulana Muhammad Rafiq Qasimi, Katibu Mkuu wa kundi la Jama't Islamiya la India, Imamu wa msikiti wa Ijumaa wa Waislamu wa Kishia mjini New Delhi Hujjatul Islam Sayyid Ali Naqawi, Mkuu wa zamani wa Akademia ya Urdu ya serikali ya India Sharif al Hasan Naqawi, na Pr. Akhtar Mahdi ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Lugha ya Kifarsi cha Chuo Kikuu cha Jawahir Lal Nehru.
Mufti Muhammad Mukarram Ahmad ambaye alikuwa mwenyekiti wa mjadala huo ametoa pongeza za kutimu miaka 30 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na juhudi za kiongozi wake hayati Imam Khomeini na akasema, uongozi wa Imam Khomeini, Mwenyezi Mungu amrehemu, na Ayatullah Ali Khamenei baada yake umewathibitishia walimwengu kwamba taifa la Iran haliiogopi Marekani na madola mengine makubwa na kwamba Imam Khomeini alihuisha Uislamu kwa kufuata nyayo za Imam Hussein (as).
Mufti Mukarram Ahmad ameongeza kuwa taifa la Iran ndilo pekee lililokuwa kigezo cha njia sahihi ya Kiislamu kati ya nchi nyingine za Kiislamu na kwamba ana matumaini Marekani na madola mengine makubwa hayatafanikiwa katika kutekeleza njama zao dhidi ya taifa hilo.
Kwa upande wake Profesa Akhtar Mahdi amesema kuwa Imam Khomeini alifanikiwa kuanzisha harakati kubwa kwa kufuata nyayo za Imam Hussein (as) ambayo imekuwa fahari kwa Waislamu wote duniani.
Maulana Muhammad Rafiq ambaye pia alihutubia kikao hicho amesema, nchi za Kiislamu zinaiogopa Marekani na kwamba ni Iran pekee ambayo imesimama kidete mbele ya dhulma za serikali ya Washington. Amesisitiza kwamba Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yaliupa Uislamu uhai mpya.
Mkuu wa Kitengo cha Utamaduni cha Iran mjini New Delhi Karim Najafi amewapongeza wananchi wa Iran kwa kutimia miaka 30 ya Mapinduzi ya Kiislamu na akasema: Imam Khomeini alipindua utawala fasidi wa Shah kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu na umoja wa wananchi kama Imam Hussein alivyosimama na kupambana na Yazid bin Muawwiya. 357350 (elimu na maarifa)