Askofu Kuryanov ambaye anaongoza ujumbe wa Wakristo wa kanisa la Orthodox la Russia katika mkutano wa mazungumzo ya dini mjini Tehran amesema kuwa mazingatio ya Qur'ani kwa misingi ya maadili bora na kanuni za maisha yanaonekana vyema katika aya nyingi za kitabu hicho na ushahidi wa wazi ni sisitizo la Qu'ani juu ya upendo udharura wa kujibu tendo baya kwa jema.
Amesema kuwa dini ya Kiislamu imetilia mkazo misingi ya maadili bora na kwamba Muislamu halisi analazimika kuwa na sifa hizo za kimaadili.
Askofu Dennis Kuryanov amesema kitabu cha Injili pia kinasheria nyingi zinazohusiana na kuwahami na kuwasaidia watu masikini na kinawausia wanadamu kutoa huduma kama hizo katika maisha yao. Amesema kuwa upendo ni msingi muhimu katika Ukristo.
Askofu Dennis Kuryanov amesisitiza kuwa dini za Uislamu na Ukristo zina mambo mengi yanayozikutanisha pamoja na kwa msingi huo zinaweza kushirikiana zaidi na kusimama kidete mbele ya mfumo wa kisekulari ambao matokeo yake ni kuporomoka thamani za kimaadili.
Mkutano wa Mazungumzo kati ya Uislamu na Kanisa la Orthoox la Russia umefanyika mjini Tehran chini ya usimamizi wa Kituo cha Mazungumzo kati ya Dini Mbalimbali. Mkutano huo umehudhuriwa na wasomi na wanafikra wa Kiislamu na Kikristo. 670407