IQNA

Maulamaa wa Kishia wa Bahrain wampongeza Sheikh wa al Azhar

17:52 - November 08, 2010
Habari ID: 2028043
Maulamaa wa kishia wa Bahrain wamemtumia ujumbe Sheikh wa al Azhar Ahmad Tayyib wakimpongeza kwa matamshi yake ya kuimarisha umoja wa Kiislamu na kutetea Waislamu wa mdhehebu ya Shia.
Wanazuoni wa Kishia wa Bahrain pia wamempongeza Sheikh Ahmad Tayyib kwa kulaani fikra na makundi yanayowakufurisha wafuasi wa madhehebu ya Ahlul Bait (as).
Taarifa iliyotolewa na Baraza la Maulamaa wa Kishia wa Bahrain imempongeza Sheikh wa al Azhar kwa matamshi yake ya kuimarisha umoja wa Kiislamu na kulaani makundi yanayowakufirisha Waislamu wa madhehebu ya Shia. Baraza hilo pia limempongeza kwa kukosoa matangazo ya baadhi ya televisheni za satalaiti.
Taarifa hiyo imesema kuwa matamshi ya Sheikh wa al Azhar ya kulaani makundi yanayowakufurisha Mashia na ukosoaji wake dhidi ya baadhi ya televisheni za satalaiti zinazowahujumu wafuasi wa Ahlul Bait wa Mtume (saw) ni hatua inayopaswa kusifiwa na kupongezwa. Taarifa hiyo imesisitiza kuwa hatua ya Sheikh Ahmad Tayyib itasaidia katika kuimarisha umoja na mshikamano kati ya Waislamu.
Baraza la Maulamaa wa Kishia wa Bahran limesisitiza katika ujumbe huo kwamba matamshi yaliyotolewa na Sheikh wa al Azhar ambcho ni kituo kikubwa cha kielimu cha Kiislamu kilichokuwa na wanazuoni wakubwa kama Sheikh Mahmoud Shaltut, si kitu cha kustaajabisha na yamewanyima fursa maadui wa umma wa Kiislamu ambao walikuwa na nia ya kuzusha fitina na mifarakano.
Maulamaa wa Bahrain wamesisitiza juu ya udharura wa umoja na mshikamano wa Kiislamu na kusema kuwa Waislamu wanapaswa kujiepusha na matamshi yanayozusha hitilafu na uhasama na kusimama pamoja kwa ajili ya kupambana na changamoto za ubeberu na Uzayuni wa kimataifa. 691363


captcha