Gazeti la Hindustan Times limendika kuwa viongozi wa kidini wa Malaysia wanawapa Waislamu wa madhehebu ya Suni peke yao uhuru wa kutekeleza ibada na hawaruhusu nadhehebu nyingine za Kiislamu kama Shia kutekeleza ibada na shughuli za kidini. Gazeti hilo limeandika kuwa madhehebu zisizokuwa za Suni kama Shia zimepigwa marufuku nchini Malaysia.
Viongozi wa Kiislamu wa Malaysia mapema mwezi huu waliwatia nguvuni Waislamu 200 wa madhehebu ya Shia waliokuwa katika maombi na dua katika eneo la katikati mwa nchi hiyo. Harakati hiyo imetambuliwa kuwa moja ya operesheni kubwa zaidi na ya aina yake ya kuwatia watu mbaroni nchini Malaysia katika miaka ya hivi karibuni.
Afisa wa Jumuiya ya Kutetea Haki za Binadamu ya Malaysia Muhammad Shani Abdullah amesema kuwa wawakilishi wa Waislamu wa madhehebu ya Shia wamewasilisha mashtaka katika jumuiya hiyo inayoungwa mkono na serikali ya Malaysia wakitaka kukomeshwa ukandaamizaji unaofanywa dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia.
Katika mashtaka hayo, Mashia wanauliza, kama dini na madhehebu nyingine za waliowachache mithili ya Wahindu, Mabudha, Wakristo na Sikh wanaruhusiwa kutekeleza ibada na shughuli zao za kidini inakuwaje Waislamu wa madhehebu ya Shia wakatazwe kufuata itikadi za mababu zao na kurushiwa tuhuma za aina mbalimbali?
Makumi ya maelfu ya raia milioni 28 wa Malaysia ni Waislamu wa madhehebu ya Shia. Baadhi ya Mashia hao wameiambia Jumuiya ya Kutetea Haki za Binadamu ya Malaysia kwamba wamelazimika kuficha itikadi zao kwa miaka mingi ili kuepuka matatizo na hawana hata maeneo ya kufanyia ibada. 720286