Tovuti ya Muhit imeripoti kuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Cordoba Abbas Urwah amesema mpango huo una lengo la kuwahutubu wanafikra na wasomi katika nchi za Magharibi ukiwataka kukabiliana na hujuma na wimbi la kuwatisha watu kuhusu dini ya Kiislamu na Waislamu.
Amesema mradi wa kuwatisha watu na kuwatia chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu unaendeshwa na watu wasiowajibika katika nchi za Magharbi ambao wanatumia vibaya migogoro ya sasa ya kimaadili, kisiasa, kiuchumi na kifedha barani Ulaya. Ameongeza kuwa watu hao wanafanya jitihada za kueneza anga ya woga na hofu kuhusu Uislamu na Waislamu katika nchi za Magharibi kupitia njama za kuzusha hali ya ukosefu wa maelewano kati ya mataifa mbalimbali.
Abbas Urwah ameongeza kuwa taasisi isiyokuwa ya serikali ya Cordoba nchini Uswisi imemtumia ujumbe Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Benedict XVI kwa kutegemea aya ya 114 ya suratun Nisaa inayosema: "Hakuna kheri kati ya mengi wanayoshauriana kwa siri isipokuwa kwa yule anayeamrisha kutoa sadaka au kutenda mema au kupatanisha baina ya watu. Na mwenye kufanya hayo kwa kutaka radhi za Mwenyezi Mungu basi tutampa ujira mkubwa."
Amesema ujumbe huo umesisitiza kuwa Waislamu kote duniani wanatarajia kuwa Papa atawataka wafuasi wa kanisa Katoliki wasikubali propaganda chafu zinazowataka wauchukie Uislamu na Waislamu, suala ambalo linazusha hitilafu na fitina katika jamii. 721826