IQNA

Ayatullah Jannati:

Harakati ya ukombozi wa Gaza inasonga mbele

12:59 - January 08, 2011
Habari ID: 2060242
Ayatullah Jannati amesema kuwa harakati za kukomboa eneo la Ukanda wa Gaza zinasonga mbele zaidi baada ya miaka mitano ya kuzingirwa eneo hilo na waovu wa dunia hii.
Khatibu wa muda wa Swala ya Ijumaa ya mjini Tehran Ayatullah Ahmad Jannati amezungumzia habari ya kuwasili msafara wa misaada ya kibinadamu wa Asia katika eneo la Ukanda wa Gaza na kusema kuwa harakati za kukomboa eneo hilo zinasonga mbele zaidi baada ya miaka mitano ya kuzingirwa eneo hilo na waovu wa dunia hii. Amesema kuwa kuwasili msafara wa misaada ya kibinadamu wa Asia katika Ukanda wa Gaza kumewafurahisha wakazi wa eneo hilo.
Ayatullah Jannati pia amewapongeza Wakristo kote duniani kwa mnasaba wa mwaka mpya na kuzaliwa Nabii Issa Masih (as) na akasema iwapo Wakristo wanataka kujua jinsi Nabii huyo wa Mwenyezi Mungu anavyoheshimiwa wanapaswa kusoma Qu’rani. Ameongeza kuwa Issa Masih hakumdhulumu mtu yeyote na kwamba Wakristo wanapaswa kumuiga Mtume huyo.
Katika upande mwingine Ayatullah Jannati amesema kuwa maadui wanaojaribu kuwachochea wananchi wa Iran ili waichukie serikali yao hawana nafasi kabisa katika jamii ya wapenda amani na maendeleo hapa nchini Iran. Ayatullah Jannati amefafanua kuwa maadui wa nchi hii walijaribu kutumia uchaguzi mkuu wa mwaka 2009 kuzusha mfarakano lakini kutokana na kuwa macho wananchi wa Iran, njama zao ziliambulia patupu. Ameongeza kuwa taifa la Iran lilitumia fursa hiyo kuwadhalilisha maadui na kwamba kuendelea kusimama kidete taifa hili pamoja na wananchi wake wapenda amani na maendeleo, kumezidi kuwatia tumbojoto maadui ambao kwa sasa wamekanganyikiwa na hawajui la kufanya. Khatibu wa muda wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran amesisitiza kuwa umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi wa Iran ndiyo silaha pekee inayoweza kumshinda adui wa nchi hii.

captcha