IQNA

Umoja wa Kiislamu unahitajia mipango ya muda mrefu

11:36 - February 23, 2011
Habari ID: 2085208
Kuthibiti kwa umoja wa Kiislamu kunahitajia mipango ya muda mrefu iliyosimama juu ya misingi ya kielimu na kiutafiti, na wanazuoni wa Kiislamu wanapasa kuongozwa na mtu kama Ayatullahil Udhma Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.
Hayo yamesemwa na Ahmad az-Zein, Mkuu wa Jumuiya ya Maulamaa wa Kiislamu ya Lebanon, ambaye amehudhuria kikao cha kimataifa cha 24 ambacho kimemalizika hivi karibuni mjini Tehran. Amesema alitoa katika kikao hicho pendekezo la kubuniwa kamati za wataalamu katika nyanja za siasa, uchumi, utamaduni, jeshi na masuala mengineyo ili ziweze kubuni ratiba za kielimu na kiutafiti kwa lengo la kuunganisha ulimwengu wa Kiislamu katika nyanja balimbali.
Amesema moja ya mambo yanayoweza kuwaunganisha Waislamu kwa msingi wa umoja na mshikamano wa Kiislamu ni kuwa na kiongozi mmoja shupavu ambaye katika zama hizi ni Ayatullahil Udhma Ali Khamenei wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Amesema Uislamu unasisitiza mno juu ya udharura wa kufanyika mashauriano na mazungumzo kati ya Waislamu kwa madhumuni ya kuimarisha umoja, udugu na mshikamano kati yao. Ameyataka mataifa yote ya Kiislamu kuimarisha umoja na udugu miongoni mwao na kujiepusha na mambo yanayoyatenganisha kwa madhara ya ulimwengu mzima wa Kiislamu.
Amesema kufanyika kila mwaka kwa vikao vya umoja wa Kiislamu ni hatua muhimu kuelekea lengo la kuunganisha ulimwengu wa Kiislamu na kubainisha matumaini yake kwamba kuhudhuria kila mwaka wanazuoni na wanafikra wakubwa wa Kiislamu katika vikao hivyo kutachangia pakubwa katika kuleta mshikamano katika ulimwengu wa Kiislamu. 752128
captcha