Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ulimwengu wa Kiislamu amewaalika maulamaa wa Kiislamu wa Iran kuhudhuria mkutano wa kimataifa wa 'Ulimwengu wa Kiislamu, Matatizo na Ufumbuzi Wake' uliopangwa kufanyika katika mji mtakatifu wa Makka.
Gazeti la al Watan la Saudi Arabia limeandika leo kuwa Abdullah bin Abdul Muhsin al Turki, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ulimwengu wa Kiislamu amesema kuwa mkutano huo wa Makka utafanyika kuanzia tarehe 23 hadi 25 Julai na wasomi na maulamaa kadhaa wa Iran wamealikwa.
Mkutano huo utasimamiwa na Amir wa Makka Sheikh Khalid Faisal. Maulamaa wa Kiislamu wa nchi za Kiarabu na Kiislamu na pia viongozi wa Waislamu wanaoishi katika nchi zisizokuwa za Kiislamu wamealikwa kuhudhuria mkutano huo.
Abdullah bin Abdul Muhsin al Turki amesema mkutano huo utajadili matatizo ya umma wa Kiislamu na njia za utatuzi wake bila ya kujadili tofauti za kimadhehebu na kikaumu. Amesisitiza kuwa Jumuiya ya Ulimwengu wa Kiislamu inakaribisha mitazamo mbalimbali hata inayotofautiana na misimamo yake. 828772