IQNA

Miaka 23 imepita tangu kuzama nyota ya kiraa ya Qur'ani

19:52 - November 30, 2011
Habari ID: 2232278
Imepita miaka 23 sasa tangu karii na msomaji mashuhuri wa Qur'ani Tukufu Ustadh Abdul Basit Abdus Samad alipoaga dunia katika ardhi ya nchi ya Misri ambayo kwa sasa inapita katika kipindi cha mabadiliko makubwa ya kuelekea kwenye demokrasia baada ya kung'olewa madarakani utawala wa kidikteta wa Hosni Mubarak mapema mwaka huu.
Ustadh Abdul Basit Abdus Samad alikuwa miongoni mwa makarii na wasomaji mashuhuri wa kimataifa wa Qur'ani Tukufu na weledi wa masuala ya Qur'ani wanamtambua kuwa ndiye karii mkubwa zaidi wa Qur'ami kote duniani. Ustadh Abdus Samad alibuni na kuanzisha mbinu makhsusi ya kiraa ya Qur'ani.
Abdul Basit Abdus Samad alizaliwa mwaka 1927 katika kijiji cha Almazaizah katika eneo la Armant katika mkoa wa Qana huko kusini mwa Misri. Babu yake, Ustadh Abdus Samad, alikuwa mtu aliyesifika kwa kuwa na takwa na uchamungu na miongoni mwa mahafidhi wa Qur'ani na vilevile mtaalamu wa masuala ya Qur'ani.
Ustadh Abdul Basit Abdus Samad alikamilisha hifdhi ya Qur'ani akiwa na umri wa miaka 10 kijijini kwake kwa Ustadh Al Amir na akahitimu aina zote za kiraa ya Qur'ani akiwa na umri wa miaka 14.
Ustadh Abdul Basit alipewa lakabu ya 'Koo ya Dhahabu' kutokana na kiraa yake ya kuvutia na alipendwa mno na wafuatiliaji wa masuala ya Qur'ani kwa kadiri kwamba hadi sasa anatambuliwa kuwa karii mashuhuri na anayepesndwa zaidi wa Qur'ani.
Ustadh alipata umashuhuri tangu akiwa kijana na kuwa msomaji anayependwa zaidi nchini Misri. Hata hivyo nyota ya karii huyo wa Kiislamu ilianza kung'ara na kupata umashuhuri zaidi nchini na katika medani ya kimataifa baada ya kushiriki katika sherehe ya maulidi ya Bibi Zainab bint Ali bin Abi Twalib (as) katika Haram ya mtukufu huyo mjini Cairo.
Tukio hilo lilijiri wakati Abdul Basit alipokuwa na umri wa miaka 19. ilikuwa mwaka 1951 wakati Ustadh Abdul Basit Abdul Samad alipokwenda mjini Cairo kwa mara ya kwanza safari ambayo ilisadifiana na mahfali kubwa iliyokuwa ikifanyika katika Haram ya Bibi Zainab (as). Baadhi ya watu waliokuwa wakimtambua Abdul Basit waliomba kusikia kiraa yake ya Qur'ani. Awali karii huyo alisita kusoma katika majlisi hiyo kutokana na kuwepo hapo makarii na wasomaji waliokuwa maarufu zaidi. Majlisi hiyo ya maulidi ilijumuisha wasomaji wakubwa kama Ustadh Abdul Fattah Sha'shaei, ustadh Abolainain Shoaisha, Ustadh Mustafa Ismail, Abdul Adhim Zahra na kadhalika.
Kwa mara ya kwanza Abdul Basit alisoma sura ya Ahzab katika majlisi hiyo kubwa ya maulidi na licha ya kwamba alipangiwa kusoma kwa dakika kumi tu lakini kiraa yake iliwavutia watu wengi waliosikika wakipiga takbira ya kumpongeza karii huyo kijana. Hali hiyo ilipelekea muda wa kisomo chake urefushwe na kuwa saa moja na nusu badala ya dakika kumi.
Mwaka 1951 Ustadh Abdul Basit Abdus Samad alianza kusoma Qur'ani redioni na kuwa miongoni mwa nyota wakubwa wa kiraa ya Qur'ani Tukufu. Tangu mwaka 1952 karii huyo mashuhuri alianza kusafiri kwenye nchi mbalimbali duniani kwa ajili ya kusoma Qur'ani katika mwezi mtukufu wa Ramadhani na minasaba mingine ya kidini.
Katika moja ya safari zake, Ustadh Abdul Basit Abdus Samad alikwenda Jakarta nchini Indonesia ambako alisoma Qur'ani katika msikiti mkubwa zaidi wa mji huo. Umati mkubwa wa watu ulifuruka ndani ya msikiti huo na nje yake kiasi kwamba hadhirina walijaa katika eneo la kilomita moja mraba kandokando ya msikiti huo na kusikiliza kiraa ya Ustadh Abdus Samad usiku kucha wakiwa wamesimama wima hadi alfajiri.
Mwaka 1952 Ustadh Abdus Samad alikwenda kuhiji Makka na kusoma Qur'ani katika Masjidul Haram na Masjidunnabi huko Madina. Vilevile alikwenda Palestina na kusoma Qur'ani huko Baitul Muqaddas na katika Haram ya Nabii Ibrahim (as).
Kiraa ya Ustadh Abdul Basit Abdul Samad iliwaathiri watu wengi na hata kuwavutia wasiokuwa Waislamu katika dini ya Kiislamu. Watu 6 waliingia katika dini ya Kiislamu baada ya kuathiriwa na kiraa yake mjini Los Angeles huko Marekani. Nchini Uganda jumla ya watu 92 walisilimu katika majlisi ya kiraa ya msomaji huyo mashuhuri na watu wengine 72 pia walikubali dini tukufu ya Kiislamu katika majlisi nyingine baada ya kuvutiwa mno na usomaji wake.
Mwishoni mwa umri wake, Ustadh Abdus Samad alipatwa na maradhi ya kisukari na baadaye uvimbe wa ini. Alipelekwa London Uingereza kwa ajili ya matibabu baada ya kuzidiwa na maradhi na kurejeshwa Cairo wiki mbili baadaye. Inasemekana kwamba Ustadh Abdul Basit Abdus Samad alikuwa amehisi kwamba siku zake za kuishi duniani zinakaribia ukingoni na wakati wa kukutana na Mola Muumba ulikuwa unakaribia.
Hatimaye tarehe 30 Novemba mwaka 1988 Ustadh Abdul Basit Abdus Samad aliaga dunia. Siku ya kufariki kwake dunia ulikuwa msiba mkubwa kwa mamilioni ya Waislamu kote duniani. Mazishi ya karii huyo mashuhuri wa Kiislamu yalihudhuriwa na maelfu ya watu wakiwemo mabalozi wa nchi mbalimbali ambao waliwakilishi nchi zao katika mazishi hayo.
Ustadh Abdus Samad alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 61. Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi. 908794



captcha