IQNA

Tarjumi ya kwanza ya Qur'ani iliyoandikwa kwa mkono yagunduliwa China

16:13 - December 17, 2011
Habari ID: 2240103
Watafiti kadhaa wa utamaduni wa Kiislamu nchini China wamegundua tarjumi ya kwanza ya Qur'ani Tukufu iliyoandikwa kwa mkono. Tarjumi hiyo ni ya lugha ya Kichina.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Xinhua la China, nuskha hiyo ya Qur'ani iliandikwa mwaka 1912 katika eneo la Guangzhou kaskazini magharibi mwa nchi.
Akibainisha suala hilo Ding Shirn Mkuu wa Taasisi ya Utamaduni wa Kiislamu amesema kuhusiana na suala hilo kwamba Qur'ani hiyo iligunduliwa na watafiti kadhaa wa taasisi hiyo ya kiutamaduni ikiwa imejificha kati ya nyaraka za kale. Amesema Qur'ani hiyo ilitarjumiwa na wanazuoni wawili mashuhuri wa Kiislamu kutoka eneo lililotajwa.
Bwana Ding amesema kuwa kuna nuskha mbili za Qur'ani ambazo zilitarjumiwa kwa lugha ya Kichina katika karne ya 20 na kwamba taasisi yake ya kiutamaduni inafanya jitihada za kuchunguza, kutathmini na kuambatanisha tarjumi tatu hizo za Qur'ani Tukufu. Amesema licha ya kuwa Uislamu uliingia nchini China kati ya mwaka 618 hadi 907 Milaadia, lakini wasomi na wanazuoni wa nchi hiyo waliogopa kutarjumu Qur'ani Tukufu wakihofia wasije wakafanya makosa katika kutafsiri maneno ya Mwenyezi Mungu.
Kabla ya kugunduliwa nuskha hiyo iliyotarjumiwa mwaka 1912 Wachina wamekuwa wakidhani kwamba tarjumi ya kwanza ya Qur'ani kwa lugha ya Kichina ni ile iliyotarjumiwa mwaka 1927 Milaadia. 916797
captcha