Akizungumza na shirika la habari za Qur'ani la IQNA Mahdi Zarei, Mkuu wa Kituo cha Dhamir amesema kuwa kituo hicho kimsingi kitakuwa kikiwasilisha vitabu na masuala mengine yanayohusiana na Qur'ani Tukufu. Amesema mambo na vitu vitakavyoonyeshwa, kutolewa, kuwasilishwa na kuuzwa kwenye kituo hicho kimsingi vitakuwa vinatoka katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Zarei amesema nchi nyingine za Kiislamu zimepiga hatua kubwa katika uwanja huo, kinyume na Iran ambayo amesema kwa masikitiko makubwa ilikuwa haijachukua hatua yoyote muhimu katika uwanja huo. Amesema jambo hilo limewapelekea wahusika kuchukua hatua ya kuanzisha Kituo cha Qur'ani cha Dhamir kwa ajili ya kushughulikia suala hilo muhimu, kituo ambacho ni cha kwanza cha Mashia kutoa huduma kama hiyo katika mji wa Guangzhou.
Akifafanua zaidi shughuli za kituo hicho cha Qur'ani Bwana Zarei amesema kuwa hakifungamani na taasisi yoyote ya serikali ya Iran bali ni cha watu binafsi ambacho kimeanzishwa kwa ushirikiano wa Wairani wanaoishi nchini Uchina. Hata hivyo amesema mashirika na taasisi za Qur'ani na Kiislamu za Iran ambazo zina hamu ya kushirikiana na kituo hicho katika kutoa huduma zao kwa Waislamu na wasio Waislamu zinaweza kufanya hivyo kwa kushirikiana nacho katika kuwasilisha bidhaa za Qur'ani na Kiislamu vikiwemo vitabu ambavyo vimechapishwa kwa lugha za Kichina, Kiingereza, Kiarabu na Kifarsi.
Amesema taasisi hizo zinaweza kuchapisha vitabu vyao nchini China kwa gharama ndogo na kushirikiana na kituo hicho katika kutuma vitabu hivyo katika pembe zote za dunia kwa muda wa siku nne tu. 917681