Kongamano hilo limefanyika chini ya anwani ya 'Qur'ani Tukufu na Nafasi Yake katika Ujenzi wa Utamaduni wa Kiislamu'. Kongamano hilo lililofunguliwa kwa hotuba ya Rais Omar al-Bashir wa Sudan katika Chuo cha Kimataifa cha Afrika lilimalizika hapo siku ya Jumamosi tarehe 17 Disemba. Wanazuoni na wasomi wa Kiislamu kutoka nchi zaidi ya 16 za dunia walishiriki katika kikao hicho.
Akizungumzia kongamano hilo, Hassan Makki, mkuu wa chuo hicho amesema kwamba zaidi ya wasomi na wanazuoni 160 walishiriki kongamano hilo na kwamba makala yote yaliyosomwa huko yamepangwa kuchapishwa katika sura ya kitabu ili kuwanufaisha watu wengine ambao hawakuhudhuria kongamano hilo.
Akizungumza katika siku ya kwanza ya kongamano hilo lililoanza siku ya Alkhamisi, Ali Othman Muhammad Taha, Makamu wa Rais wa Sudan amesisitiza juu ya kulindwa umoja na mshikamano wa Waislamu kwa kuzingatiwa misingi na mafundisho ya kitabu kitakatifu cha Qur'ani Tukufu.
Amewataka wasomi na wanazuoni wa Kiislamu kuishawishi jamii iheshimu na kufuata mafundisho ya Qur'ani. Amesema watu wanapasa kuzingatia mafundisho ya kitabu hicho kitakatifu ili kufanikiwa katika maisha yao ya humu duniani na ya huko Akhera. 918347