IQNA

Wito wa kukusanywa nuskha za Qur'ani kwa ajili ya kutumwa Afrika

10:36 - December 26, 2011
Habari ID: 2245259
Taasisi ya Mambo ya Kheri ya Yumn ya Misri imetoa wito wa kukusanywa nuskha za Qur'ani Tukufu zisizotumika majumbani kwa ajili ya kutumwa katika nchi tofauti za kusini mwa Afrika.
Taasisi hiyo imetoa wito huo kupitia taarifa ambapo imewataka Waislamu kukusanya nuskha hizo za ziada zisizotumika katika nyumba zao na kuwezesha kutumwa katika nchi za kusini mwa Afrika ambazo zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa nuskha hizo misikitini. Imesema Waislamu wa nchi hizo wanalazimika kusoma Qur'ani moja kwa makundi kutokana na uhaba wa kitabu hicho misikitini.
Taasisi ya Yumn inasema watu wanaosilimu katika nchi hizo hawana fursa ya kunufaika na Qur'ani Tukufu kutokana na uhaba wa nakala za kitabu hicho cha wahyi ni pia ughali wake katika nchi hizo.
Imesema watu wote wanaweza kushiriki katika mpango wa kukusanya na kutuma nuskha za Qur'ani katika nchi za kusini mwa Afrika na kwamba wanaweza pia kununua nuskha mpya za Qur'ani kwa lengo hilohilo.
Taasisi hiyo ya Misri imesema kwamba hata kama jambo hilo litaonekana kuwa dogo na lisilo na umuhimu mkubwa kwa wengi lakini ni lenye thamani kubwa mbele ya Waislamu wa Afrika wanaokabiliwa na uhaba wa nakala za kitabu hicho cha mbinguni.
Taasisi ya Yumn inajishughulisha na masuala mbalimbali ya kuwasaidia mayatima wanaohitaji misaada katika nchi tofauti za dunia. Hutembelea na kusaidia kwa karibu pia wagonjwa wanaokabiliwa na maradhi mbalimbali maalumu na sugu. 922190
captcha