Viongozi wa ngazi za juu wa ANC wamewataka wananchi wa Afrika Kusini kufanya kila wawezalo kuushinikiza utawala wa Israel ili ukomeshe uvamizi wake huko Palestina. Hivi karibuni serikali ya Pretoria ilijiunga rasmi kwenye kambi ya wapinzani wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Vuilevile wabunge wa bunge la nchi hiyo wamelitaja jeshi la utawala wa Israel kuwa linatenda ukatili na unyama kuliko ule uliokuwa ukifanywa na utawala wa makaburu nchini humo. Wapinzani wa Israel huko Afrika Kusini, mara kadhaa wamekuwa wakitoa nara zinazotaka kuwekewa vikwazo utawala ghasibu wa Israel, kusitishwa uwekezaji katika iradi mbalimbali ya utawala huo na kusisitiza juu ya kukatwa mashirikiano ya kiuchumi na Wazayuni.
Dosari zilizojitokeza sasa kwenye uhusiano wa Pretoria na Tel Aviv siyo jambo geni. Kwani uhusiano kati ya pande hizo mbili ulianza kuingia dosari baada ya kuchaguliwa Nelson Mandela kuwa Rais wa Kwanza mweusi nchini Afrika Kusini mwaka 1994. Mandela alifuta makubaliano yote ya kijeshi na utawala huo haramu na badala yake akawa bega kwa bega na wananchi wa Palestina.
Viongozi wa Afrika Kusini mwezi Agosti mwaka huu waliamuru kwamba bidhaa zinazotengenezwa Israel ziandikwe juu yake kwamba zimetengenezwa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina badala ya Israel. Hali kadhalika mara kadhaa serikali ya Afrika Kusini imekuwa ikisisitiza juu ya kutekelezwa azimio la Umoja wa Mataifa la mwaka 1948, ambalo halitambui rasmi mipaka iliyowekwa na Wazayuni katika ardhi wanazozikalia kwa mabavu za Palestina baada ya mwaka huo. Kupigwa marufuku matangazo ya kibiashara ya bidhaa zinazotengenezwa Israel, ni suala lengine ambalo limezidi kuwakera Wazayuni na kutia dosari uhusiano wa pande hizo mbili. Misimamo hiyo imara ya viongozi wa Afrika Kusini, imekabiliwa na radiamali kali kutoka kwa Wazayuni. Viongozi wa Israel wanadai kuwa, misimamo ya viongozi wa Pretoria ni ya kibaguzi.
Weledi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa, maazimio yaliyopitishwa hivi karibuni nchini Afrika Kusini, ikiwa ni nchi yenye nguvu kubwa ya kiuchumi barani Afrika, kwa hakika yamedhoofisha nafasi ya utawala wa Israel katika bara hilo; kwani eneo hilo ni moja kati ya maeneo yanayozingatiwa na kupewa umuhimu sana na utawala wa Israel hasa katika siasa za kigeni za utawala huo. Weledi hao wanaeleza kuwa, Wazayuni wanasisitiza juu ya kuimarisha shughuli za kibiashara na kiuchumi barani Afrika kutokana na sababu mbalimbali za kiusalama na kiuchumi.
Kwa upande mwengine, ukuaji wa kasi wa dini ya Kiislamu barani Afrika, ni maudhui nyingine inayowatia kiwewe Wazayuni. Nchi za Kiafrika pia zina umuhimu wa kiistratijia kwa utawala huo ghasibu. Utawala wa Israel unafanya njama za kuchochea hitilafu za kikaumu na kikabila na kuzusha migogoro na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, ili uweze kuimarisha satua na ushawishi wake kwenye maeneo ya kiistratijia kama barani Afrika.
1159812