Duru za habari zinasema kuwa takwa la Mkurugenzi wa Mashtaka wa Saudia la kuhukumiwa kifo mwanazuoni huyo mashuhuri limekabiliwa na tahadhari kali ya Waislamu wa madhehebu ya Shia na kambi ya upinzani.
Kambi ya wapinzani wa serikali ya Riyadh imetangaza kuwa, hukumu ya kifo dhidi ya msomi huyo wa Kiislamu itakuwa kosa na jinai kubwa na imetahadharisha kuwa maeneo ya Mashariki mwa Saudi Arabia yenye idadi kubwa ya Waislamu wa madhehebu ya Shia yatawaka moto iwapo mahakama itatoa hukumu kama hiyo.
Tayari vipeperushi vimeanza kuenezwa katika maeneo ya mashariki mwa Saudia vikiutahadharisha utawala wa kifalme wa nchi hiyo kwamba utakabiliana na harakati za kulipiza kisasi iwapo msomi huyo atahukumiwa kifo. Vilevile wakazi wa maeneo yenye utajiri mkubwa wa mafuta ya mashariki mwa Saudi Arabia wametahadharisha kuwa hawataruhusu mafuta ya eneo hilo kusafirishwa nje na kwamba Marekani inawajibika kulinda maisha ya mwanazuoni huyo kwa sababu ndiyo inayowalinda watawala wa kifalme wa Saudia.
Mkurugenzi wa Mashtaka wa Saudi Arabia ameitaka mahakama ya nchi hiyo imhukumu adhabu ya kifo Ayatullah Sheikh Namer Al Namer kwa tuhuma eti za kuchochea ugaidi.
Msomi huyo wa Kiislamu alifungwa katika seli ya mtu mmoja tangu miezi nane iliyopita kwa tuhuma za kuchochea fitina na ghasia katika maeneo ya mashariki mwa Saudia. 1207098