IQNA

Mwanazuoni wa Kishia auawa shahidi Uganda, serikali kuchunguza

13:51 - December 29, 2014
Habari ID: 2646978
Kiongozi mwandamizi wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Uganda Sheikh Ductoor Abdul Qadir Sudi Muwaya aliuawa shahidi Alkhamisi iliyopita. Mkuu wa polisi nchini humo ametangaza kuwa uchunguzi wa kina utafanyika kubainisha aliyetekeleza mauaji hayo.

Shahidi Sheikh Abdul Qadir ambaye alikuwa muasisi na mkurugenzi wa Taasisi ya Kiislamu ya Ahlul Bait  AS alipigwa risasi siku ya Alkhamisi na watu wasiojulikana mbele ya nyumba yake muda mfupi tu baada ya kuswali sala ya Ishaa na kusoma  Dua Kumayl katika msikiti wa Buyemba.
Jenerali Kale Kayihura, Mkuu wa Polisi ya Uganda ambaye amesisitiza kuwa, hataondoka katika Wilaya ya Mayuge hadi watu waliomuua kiongozi huyo wa Waislamu wa Kishia watakapotiwa mbaroni.
Shahid Ductoor Abdul-Qadir ambaye katika uhai wake amewahi kufanya kazi na gazeti lililowahi kupata umashuhuri mkubwa la Sauti ya Umma lililokuwa likichapishwa nchini Iran na kutarjumu pia vitabu kadhaa alijipatia umashuhuri mkubwa sio katika Wilaya yake tu ya Mayuge bali hata katika maeneo mengine ya Uganda kutokana na harakati zake za kidini na za kimaendeleo. Akiwa kiongozi wa Taasisi ya Kiislamu ya Ahlul Bait (ABIF) marhumu Sheikh Abdul Qadir ambaye alifahamika zaidi kwa jina la Doktoor Abdul Qadir alisimamia ujenzi wa misikiti 70, shule zaidi ya 40 na kumbi za kidini zijulikanazo kama Husseiniya katika maeneo mbalimbali nchini Uganda. Aidha alidhamini gharama za masomo kwa watoto wasio na uwezo. Shahid Abdul Qadir alizikwa siku ya Ijumaa katika Wilaya ya Mayuge mashariki mwa Uganda katika mazishi yaliyohudhuriwa na maafisa mbalimbali wa serikali na wa kiusalama akiwemo Mkuu wa jeshi la Polisi nchini Uganda…/mh

2640339

captcha