IQNA

Walimwengu waendelea kulaani kuvunjiwa heshima Mtume Muhammad SAW

11:11 - January 26, 2015
Habari ID: 2766561
Waislamu na hata wasiokuwa Waislamu duniani wanaendelea kulaani kitendo cha hivi karibuni cha jarida moja la Ufaransa la Charlie Hebdo kuchora vibonzo vinavyomvunjia heshima Mtumu Mtukufu wa Uislamu, Mohammad SAW.

Hapo jana  kote Iran kulikuwa na mijimuiko mikubwa ya wananchi chini ya nara ya "Mimi Ninampenda Mohammad SAW". Mijimuiko hiyo ya kudhihirisha mahaba ya dhati kwa Bwana Mtume SAW ilifanyika katika maeneo matakatifu na misikiti kote Tehran na miji yote mikubwa ya Iran. Katika vikao hivyo vya adhuhuri, baada ya sala ya jamaa washiriki walisoma Qur'ani Tukufu na kufuatiwa na hotuba za wanazuoni kuhusu shakhsia aadhimu ya Mtume Mtukufu wa Uislamu SAW. Aidha katika hotuba hizo, hadhirina walifahamishwa kuhusu njama za maadui ambao wanataka kueneza hofu na chuki dhidi ya Uislamu duniani kote duniani. Aidha jana Jumapili kulifanyika kikao cha kila mwaka cha  taasisi zote zinazoandaa sherehe za Alfajiri 10 za maadhimisho ya mwaka wa 36 wa Uishindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Baada ya kikao hicho, washiriki kutoka kote Iran walitoa taarifa na kulaani vikali hatua ya Wamagharibi kumvunjia heshima Mtume Mtukufu wa Uislamu SAW.
Kwingineko duniani wananchi wa kawaida, wasomi, taasisi za Kiislamu na Kikristo zimetoa taarifa mbali mbali kulaani vikali jarida la Kifaransa la Charlie Hebdo kutokana na hatua yake ya kuchapisha vibonzo  vinavyomvunjia heshima Mtume Muhammad SAW.  Kwingineko Wapalestina wamelaani vikali kitendo cha chuki dhidi ya Uislamu cha Avidgor Liebermann waziri wa mambo ya nje wa utawala haramu wa Israel ambaye amesambaza jarida la kishenzi la Charlie Hebdo katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Kamati wa Wananchi Wanamapambano Palestina imetangaza kuwa, hatua ya Liebermann kusambaza kwa wingi jarida la Kifaransa lililomvunjia heshima Mtume SAW katika ardhi za Palestina zinazozkaliwa kwa mabavu ni vita vya wazi vya kidini vya adui Mzayuni dhidi ya Waislamu wa Palestina na matukufu yao.
Aidha maelfu ya Wapalestina wameandamana katika Ukanda wa Ghaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kulaani hatua zote za chuki dhidi ya Uislamu duniani. Halikadhalika maandamano na malalamikio yanaendelea kushuhudiwa katika nchi za Asia kama vile Pakistan, Afghanistan, Indonesia, Bangladesh, Malaysia n.k ambapo Waislamu wamelaani vikali vitendo vyote vya kuvunjiwa heshima matukufu ya kidini. Katika nchi za Afrika kama vile Tanzania, Kenya, Uganda, Nigeria, Kodivaa, Morocco na Senegal Waislamu  wamelaani vikali vitendo vyovyote vya kuvunjiwa heshima Mtume SAW.  Maandamano katia  baadhi ya nchi hizo yamefanyika mbele ya balozi za Ufaransa. Naye Ayman Mazyek  Katibu Mkuu  wa Baraza Kuu la Waislamu Ujerumani katika mahojiano na jarida la kila wiki la nchi hiyo la Focus amesema kufuatia hujuma dhidi ya Jarida la Charlie Hebdo mjini Paris, Waislamu Ujerumani na hasa wanawake wanaovaa Hijabu wamekuwa wakihangaisha sana mitaani.
Ikumbukwe kuwa hivi karibuni Jarida la Charile Hebdo lenye chuki za muda mrefu dhidi ya Uislamu na Waislamu lilichapaisha vibonzo vya kumvunjia heshima Mtume Mtukufu wa Uislamu, Mohammad SAW. Mwaka 2011 jarida hilo la Ufaransa pia lilichapisha vikatuni vilivyomvunjia heshima Mtume Mtukufu wa Uislamu Muhammad SAW.../mh

2762106

captcha