IQNA

Maelfu wahudhuria mazishi ya Waislamu waliouawa Marekani

20:50 - February 13, 2015
Habari ID: 2846215
Maelfu ya watu wamehudhuria mazishi ya wanachuo watatu Waislamu ambao waliuawa kwa kupigwa risasi katika mji wa Chapel Hill jimbo la Carolina Kaskazini.

Wanafunzi wa vyuo vikuu na wakaazi wa mji wa Chapel Hill wameshiriki katika mijumuiko mikubwa kuwakumbuka wanafunzi hao waliouawa kigaidi.
Siku ya Jumanne wanafunzi watatu Waislamu nchini Marekani walipigwa risasi na kuuawa kigaidi katika jimbo la Carolina Kaskazini. Maafisa wa usalama wanasema wanafunzi hao Waislamu raia wa Marekani walipigwa risasi katika nyumba yao iliyoko karibu na Chuo Kikuu cha Carolina Kaskazini. Waliouawa ni Bw. Deah Shaddy Barakat aliyekuwa na umri wa miaka 23, mke wake Yusor Mohammad Abu-Salha aliyekuwa na miaka 21 na dada yake Razan Mohammad Abu-Salha aliyekuwa na miaka 19. Polisi wametangaza kuwa wamemtia mbaroni gaidi aliyefanya jinai hiyo aliyetambuliwa kwa jina la Craig Stephen Hicks. Chris Blue mkuu wa polisi mjini Chapel Hill ameshiriki mazishi ya Waislamu hao waliouawa kigaidi na kusema uchunguzi utafanyika kubaini iwapo mauaji hayo yalifanyika kutokana na chuki za kidini au la. Naye Mohammad Mohammad Abu-Salha  baba ya wanawake wawili waliouawa ambao wana asili ya Palestina amesema chuki dhidi ya Uislamu ndiyo sababu kuu ya mauaji ya wanafunzi hao watatu. Katika mahojiano na Press TV, Kasisi Mark Dankof mkaazi wa San Antonio, Texas, Marekani amesema, mauaji ya wanafunzi hao watatu Waislamu ni matokeo ya uchochezi wa vyombo vya habari vya Marekani vinavyoeneza taswira isiyo sahihi ya Waislamu. Amesema huku upelelezi ukiendelea, kilicho wazi ni kuwa jinai hiyo imetokana na chuki. Jana Alkhamisi wanaharakati wa kijamii walikusanyika katika eneo la mauaji ya Waislamu hao chini ya nara za 'Mwamako Dhidi ya Ubaguzi wa Rangi', 'Umoja Dhidi ya Ufashisti (UAF)' na 'Ajira na Ustawi kwa Waislamu.' Aidha wanaharakati hao wamevituhumu vyombo vya habari vya Magharibi kuwa vinafuata sera za kindumakuwili sambamba na kueneza chuki dhidi ya Waislamu.


Pamoja na kuwa Waislamu hao watatu wameuawa kigaidi huko Carolina Kaskazini nchini Marekani, lakini tumeshuhudia kunyamaza kimya au kupuuzwa na kufifilizwa habari hiyo katika aghlabu ya vyombo vya habari vya Marekani na nchi zingine za Magharibi. Pamoja na hayo kuhudhuria maelfu ya watu katika mazishi ya wanafunzi hao watatu Waislamu na pia jumbe mbali mbali zilizotumwa katika mitando ya kijamii ni jambo linaloashiria ufa mkubwa uliopo baina ya aghlabu ya vyombo vya habari vya Magharibi na wananchi. Ni vyombo vichache tu vya habari vilivyoakisi kwa njia sahihi habari ya mauaji ya kigaidi ya Waislamu hao. Hapa tunaweza kuangalia mifano miwili ya namna vyombo vya habari vya Kimagharibi vilivyoakisi habari ya kuuawa kigaidi Waislamu hao watatu na hujuma za hivi karibuni huko Paris hasa dhidi ya jarida la Charlie Hebdo. Televisheni ya Fox News katika kutangaza habari ya mauaji ya Chapel Hill iliridhika kutangaza tu kuwa 'mtu moja ametuhumiwa kuwaua Waislamu watatu'. Televisheni hii hii iliakisi kikamilifu matamshi ya Rais Obama wa Marekani kufuatia hujuma dhidi ya Charlie Hebdo mjini Paris na kuitaja hujuma hiyo kuwa 'ugaidi wa kuogofya.' Televisheni ya CNN nayo pia imemtaja mtu aliyewaua Waislamu hao watatu kuwa ni mtuhumiwa tu katika hali ambayo bila ya uchunguzi wowote iliwataja kuwa magaidi waliofanya hujuma ya Charlie Hebdo. Aidha itakumbukwa kuwa punde baada ya tukio la Charlie Hebdo, vyombo vya habari na viongozi kadhaa wa Magharibi waliwashinikiza Waislamu waombe msamaha kutokana na tukio hilo sambamba na kulilaani lakini hivi sasa hatuoni kundi lolote likitakiwa kulaani au kuomba msamaha kutokana na jinai dhidi ya Waislamu huko Chapel Hill. Hivyo tukizingatia kwa kina tutaona kuwa vyombo vya habari vya Maghairbi vimetafautisha katika upashaji habari kuhusu matukio mawili ya Charlie Hebdo na Chapel Hill. Kilicho wazi ni kuwa vyombo vya habari vya kimagharibi havijaakisi ipasavyo hujuma ya kigaidi dhidi ya Waislamu katika mji wa Chapel Hill wa jimbo la Carolina Kaskazini nchini Marekani.../mh

2844147

captcha