Wakaazi wa mji huo wamenukuliwa wakisema kuwa katika jinai hiyo Jumanne iliyopita, magaidi waliwaua kwa umati watu wasiopungua 68 wengi wao wakiwa vijana na watoto waliokuwa wamekusanyika katika kikao cha kusoma Qu'rani. Mashuhuda wanasema Boko Haram walitumia silaha mpya kabisa katika kuzingira kikao hicho cha kusoma Qur'ani Tukufu na wakawafyatulia risasi kiholela waliokuwa hapo. Seneta wa eneo hilo Ali Nduwe amenukuliwa akisema kuwa magaidi wa Boko Haram waliuvamia mji huo wa Gwoza siku chache zilizopita na kuwaua wanaume huku wanawake na watoto wakilazimika kuyakimbia makazi yao.
Huku hayo yakijiri kinara wa Boko Haram ametangaza utiifu wake kwa kundi la kigaidi la Daesh (ISIL) Abubakr Shekau ametangaza kupitia mtandao wa kijamii wa tiwtter kuwa anamtii kiongozi wa kundi la kitakfiri la Daesh, Abubakr Baghdad. Katika siku za hivi karibuni magaidi wa Boko Haram wamekuwa wakitekeza jinai na ukatili sawa na ule wa kundi la Daesh kama vile kuwachinja na kuwateketeza moto watu wasio na hatia. Neno Boko Haram kwa ya lugha ya Kihausa lina maana ya 'elimu kutoka nchi za Magharibi ni haramu'. Zaidi ya watu elfu 13 wamepoteza maisha nchini Nigeria tokea kundi la Boko Haram lianzishe uasi mwaka 2009. Boko Haram ni kundi lenye misimamo ya kufurutu mipaka nchini Nigeria ambalo kutokana na kuwa na ufahamu mbaya na potofu kuhusiana na Uislamu, limeitumbukiza nchi hiyo katika dimbwi la machafuko na mauaji sambamba na kuzusha hitilafu za kidini na kikabila.../mh