IQNA

Boko Haram watekeleza mauaji ya umati dhidi ya Waislamu Nigeria

23:26 - July 03, 2015
Habari ID: 3322598
Zaidi ya Waislamu 150 wameuawa katika mashambulio ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram kaskazini mwa Nigeria.

Imeripowia kuwa, wanamgambo wa kundi la kigaidi la Boko Haram jana Alkhamisi waliwavamia wananchi katika vijiji kadhaa vya kaskazini mashariki mwa Nigeria na kuua zaidi ya wanavijiji 150 wakiwemo wanawake na watoto wadogo wakiwa majumbani mwao bali hata waliokuwa wanasali misikitini. Walioshuhudia wanasema kuwa makumi ya wanamgambo wa Boko Haram waliwamiminia risasi kiholela wakazi wa vijiji vitatu vya mbali vya jimbo la Borno na hayo yanahesabiwa kuwa ni mauaji makubwa zaidi ya umati tangu alipoingia madarakani Rais Muhammadu Buhari wa nchi hiyo. Ripoti zinasema  Waislamu 97 waliuawa kwa umati katika kijiji kimoja pekee cha Kukawa wakiwa ndani ya msikiti wakati wa magharibi walipokuwa wakifuturu baada ya sawm ya siku hiyo ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Mtu mmoja aliyeshuhudia mauaji hayo ya umati amesema kuwa, wanamgambo waliofanya ukatili huo walikuwa ni zaidi ya 50. Baada ya kutokea mauaji hayo ya umati, serikali ya Nigeria imetangaza hali ya hatari kwenye eneo hilo zima na kuwatia mbaroni zaidi ya watu 60 kwa tuhuma za kushirikiana na kundi la kigaidi la Boko Haram. Mauaji hayo ya kigaidi yametokea katika hali ambayo Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria ameongeza mapambano yake dhidi ya genge la Boko Haram na kuahidi kulitokomeza kundi hilo nchini Nigeria. Wakati wa kampeni za uchaguzi, Buhari aliwaahidi wananchi wa Nigeria kuwa atapambana vikali na genge hilo na kuwataka waisaidie serikali yake iwapo angelichaguliwa kuongoza nchi hiyo. Mara baada ya kuingia madarakani, Rais Buhari alichukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuongeza nguvu za kijeshi katika jimbo la Borno, la kaskazini mashariki mwa Nigeria ambalo linahesabiwa kuwa ni ng'ome ya kundi la Boko Haram. Hata hivyo, hivi sasa zaidi ya mwezi unapita tangu hatua hizo zichukuliwe lakini bado wananchi wa Nigeria wanashuhudia mashambulio ya kigaidi ya Boko Haram. Hii ni katika hali ambayo zaidi ya watu mia moja wameuawa katika mlolongo wa miripuko ya mabomu ya wiki za hivi karibuni kwenye mji wa Maiduguri, makao makuu ya jimbo la Borno. Mbali na kuongeza nguvu za kijeshi kwenye jimbo hilo, Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria hivi majuzi ametoa amri ya kuundwa mungano wa pamoja wa kijeshi wa kupambana na Boko Haram. Vilevile katika kikao cha mjini Johannesburg, Afrika Kusini, Buhari alitangaza kutenga dola milioni 21 kwa ajili ya vikosi vya kupambana na Boko Haram. Wachambuzi wa mambo wanaamini kwamba, ijapokuwa Buhari amechukua hatua kadhaa muhimu katika kipindi hiki kifupi cha kuingia kwake madarakani lakini inaonekana kuwa hatua kubwa zaidi, nia ya kweli na fedha nyingi zaidi zinahitajika kwa ajili ya kulitokomeza genge hilo la kigaidi. Hivi sasa genge la Boko Haram limeshadidisha mashambulio yake katika maeneo ya kaskazini na mashariki mwa Nigeria na pia katika nchi jirani kama vile Chad jambo ambalo linaonesha kuwa hatari ya genge hilo haiko tu nchini Nigeria. Weledi wa mambo wanaonya kuwa, kama hakutachukuliwa hatua za maana za kupambana na wanamgambo wa Boko Haram huko kaskazini mashariki mwa Nigeria na kwenye mipaka ya nchi hiyo na nchi jirani, basi hatari za genge hilo la kigaidi zitaenea katika bara zima la Afrika.../mh

3322494

captcha