Sayyid Hassan Nasrullah amesema hayo katika hotuba yake kwenye mahafali ya wahitimu wa masomo ambao ni watoto wa mashahidi wa muqawama na kubainisha kwamba, Hizbullah inatangaza kwa fakhari kwamba, inashirikiana na vikosi vya Syria kwa ajili ya kuzuia upenyaji wa makundi ya kigaidi katika ardhi ya Lebanon na natija ya ushirikiano huo ni kushindwa mtawalia magaidi hao.
Katibu Mkuu wa Hizbullah ameongeza kuwa, ushirikiano wa wapiganaji wa harakati hiyo na jeshi la Syria umepelekea kusambaratika njama za maadui na kushindwa mipango yao ya kuuondoa madarakani utawala wa rais Bashar al-Assad na kuisambaratisha kambi ya muqawama na mapambano. Aidha Sayyid Hassan Nasrullah amezungumzia matukio ya Lebanon na kuelezea wasi wasi wake alionao kutokana na kubakia wazi kiti cha urais na kuongeza kuwa, nchi hiyo haipaswi kuwa katika hatari ya pengo la kisiasa kwani hali hiyo inaipeleka nchi katika hatima na majaaliwa yasiyojulikana.../mh