IQNA

Nakala ya Qur’ani yapatikana katika mabaki ya ndege ya Malaysia

12:48 - August 08, 2015
Habari ID: 3340026
Nakala ya Qur’ani Tukufu iliyofunikwa kwa plastiki imepatikana katika viswa vya Reunion Bahari ya Hindi na inaaminika kuwa inafungamana na mabaki ya ndege ya Malaysia iliyotoweka mwaka jana.

. Katika siku za hivi karibuni kumepatikana mabaki kadhaa ya ndege ya Boeing ya Malaysia ambayo yameibuka katika ufukwe wa kisiwa cha Reunion kinachomilikiwa na Ufaransa mashariki mwa Afrika. Mwandishi habari wa Malaysia amesema nakala hiyo ya Qur’ani imeandikwa kwa hati za Kiarabu zijulikanazo kama Jawi, ambazo hutumika sana Malaysia, Indonesia, Brunei na eneo lenye Waislamu wengi la Mindano nchini Ufilipino. Wakaazi wa Reunion wameipata nakala hiyo ya Qur’ani Ijumaa na kuikabidhi kwa maafisa husika. Siku chache zilizopita kulipatikana matumaini ya kubainika hatima ya ndege ya Malaysia iliyotoweka zaidi ya siku 500 zilizopita baada ya Wizara ya Uchukuzi ya Malaysia kutangaza kuwa mabaki ya ndege yaliyogunduliwa kwenye ufukwe wa kisiwa cha Reunion yamethibitishwa kuwa ni sehemu ya ndege ya abiria aina ya Boeing 777.

Ndege hiyo ilitoweka tarehe nane mwezi Machi mwaka 2014 baada ya kuondoka Kuala Lumpur, Malaysia ikielekea Beijing, China ikiwa na watu 239. Ndege hiyo ilisadikiwa kuwa imeanguka baharini na hivyo ilitafutwa bila mafanikio katika eneo kubwa la Bahari ya Hindi.

3339873

captcha