IQNA

Qur’ani kwa dhahabu na rangi: Msanii wa Kiirani atafakari Sanaa ya Tadhib

15:18 - May 25, 2025
Habari ID: 3480736
IQNA – Msanii mmoja kutoka Iran ameielezea namna uzuri wa kiroho wa Qur’an Tukufu unavyoendelea kumvutia na kumtia hamasa katika kazi yake ya sanaa ya kitamaduni ya tadhib au tazhib (mapambo ya Qur’an kwa dhahabu), ambayo ni miongoni mwa sanaa za Kiislamu za kale zinazotumika kupamba kurasa za Qur’an Tukufu.

“Kila ninapotazama aya za Qur’an, uzuri wa maneno ya Mwenyezi Mungu hunidhihirikia kupitia sanaa ya tazhib,” alisema Parvaneh Kaviani, mshindi wa kitengo cha tazhib katika Tamasha la 29 la Qur’an na Etrat, lililoandaliwa na Wizara ya Afya ya Iran na kuandaliwa na Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba cha Zanjan wiki hii.

Kaviani aliongeza kuwa Qur’an daima imekuwa msingi wa safari yake ya kisanii. “Qur’an ndiyo chanzo cha mwendo wa kalamu yangu.”

Akizungumza na IQNA, Kaviani alisema kuwa kushiriki katika tamasha hilo ni fursa ya kipekee ya kutafakari, kimawazo na kiroho. “Tamasha hili ni nafasi ya kuwa peke yako na nafsi yako, ukiwa na Qur’an na sanaa. Kila mpigo wa brashi huendana na mapigo ya moyo wangu kwa sauti ya Wahyi (ufunuo), na kila rangi huakisi mnong’ono wa kutoka mbinguni.”

Alibainisha kuwa amekuwa mshiriki wa tamasha hilo kila mwaka tangu 2014, na amekuwa akipata tuzo na kutambuliwa mara kwa mara. Kwa mujibu wa Kaviani, uzoefu huu umeimarisha muunganiko wake wa kiroho na kupanua mtazamo wake kuhusu maisha, sanaa, na hata majukumu yake ya kitaaluma.

Alifafanua kuwa tazhib ni sanaa ya kale iliyo na mizizi katika utamaduni wa Kiirani-Kiislamu. Inatumia michoro ya maua na maumbo ya kijiometria kupamba kingo za maandiko ya Qur’an Tukufu. Sanaa hii huhitaji subira, umakini mkubwa, na moyo wa ibada. “Kila kazi ni kielelezo cha imani, ubunifu, na heshima kwa ujumbe wa Mwenyezi Mungu,” alisema.

“Sanaa na Qur’an ni nyuso mbili za sarafu moja,” Kaviani alihitimisha. “Moja huugusa moyo kwa uzuri, na nyingine huihuisha roho kwa maana. Kwa pamoja, huongoza mtu kuelekea kwenye kujitambua kwa kina na kumjua Muumba kwa undani zaidi.”

3493207

captcha