Kiongozi Muadhamu ameyasema hayo hii leo alipokutana na watu wa matabaka mbalimbali wakazi wa mkoa wa Chaharmahal na Bakhtiari, kusini magharibi mwa nchi na kuongeza kuwa, mazungumzo ni njia ya nchi hiyo ya Magharibi kujipenyeza na kulitwisha taifa hili matakwa yake na kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliafiki kushiriki mazungumzo ya nyuklia kwa sababu maalumu. Akiashiria kuwa, wawakilishi wa taifa hili katika mazungumzo hayo walikuwa na nafasi chanya, amesema kuwa Iran haijaruhusu kujadiliana na Marekani kuhusu masuala mengine na wala haitofanya hivyo. Aidha Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesisitiza juu ya uchumi wenye nguvu na wa muqawama, maendeleo ya elimu na roho ya Mapinduzi, kama mambo matatu yatakayoimarisha uwezo wa taifa la Iran katika kukabiliana na maadui na kuongeza kuwa, ni wadhifa wa viongozi wa nchi kuwalea vijana kwa ajili ya kulinda Mapinduzi. Amesema kuwa, kuhitimishwa maslahi ya Washington nchini Iran kwa kuondolewa utawala wa Kipahlavi, ndio sababu ya kuendelea chuki na uadui dhidi ya taifa hili na kuongeza kuwa, haipaswi kutolewa mwanya wowote wa kuruhusu kurejea tena Wamarekani nchini hapa. Akiashiria kuwa, uadui wa Marekani dhidi ya taifa hili ni jambo lisilo na ukomo amesema, hata katika hali ambayo bado kunasubiriwa kufikiwa makubaliano ya pamoja ambayo hadi sasa hayajaeleweka mustakbali wake hapa nchini na Marekani, viongozi wa Washington wameendelea kujishughulisha na jinsi ya kutekeleza njama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu kupitia kongresi ya nchi hiyo.../mh