IQNA

Nasrallah asisitiza mapambano dhidi ya njama za US, Israel

14:26 - October 25, 2015
Habari ID: 3393522
Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesisitiza juu ya udharura wa kuendelezwa mapambano dhidi ya njama za Marekani, utawala ghasibu wa Israel na matakfiri katika Mashariki ya Kati.

Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesisitiza juu ya udharura wa kuendelezwa mapambano dhidi ya njama za Marekani, utawala ghasibu wa Israel na matakfiri katika Mashariki ya Kati. Sayyid Hassan Nasrallah aliyasema hayo Jumamosi katika hotuba yake kwenye mabombolezo ya Siku ya Ashura kusini mwa Beirut Lebanon na kuzitaka nchi na mataifa yote ya Kiislamu na Kiarabu kutekeleza majukumu yao ipasavyo katika kuwalinda wananchi na kutoa himaya na uungaji mkono kwa muqawama wa Palestina na mapambano yao ya kutetea Quds na msikiti mtakatifu wa al-Aqswa kibla cha kwanza cha Waislamu. Kiongozi huyo wa Hizbullah amesema ana matarajio njama kama za matakfiri na za utawala wa Kizayuni wa Israel zitashindwa. Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon ameyataka makundi ya kisiasa nchini Lebanon yafikie maafikiano ya kuyatafutia ufumbuzi matatizo ya nchi hiyo. Sayyid Nasrallah amelaani vikali uvamizi wa Saudi Arabia dhidi ya Yemen na kuongeza kuwa, ni fakhari kubwa kutoa himaya na uungaji mkono kwa muqawama wa Yemen, jeshi na kamati za wananchi wa nchi hiyo. Kuhusiana na maafa ya Mina, Sayyid Nasrallah amesema, Mahujaji waliopoteza maisha katika maafa hayo wamekuwa wahanga wa uongozi mbovu na uzembe wa viongozi wa Saudia katika kusimamia ibada ya Hija.
Nasrallah: Marekani inataka kudhibiti Mashariki ya Kati
Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa Marekani ambayo imerithi ukoloni wa zamani inafanya mikakati ya kulidhibiti kikamilifu eneo la Mashariki ya Kati.
Sayyid Hassan Nasrallah aliyasema hayo Ijumaa usiku mjini Beirut katika mkesha wa tarehe 10 Muharram na kumbukumbu ya kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) Imam Hussein (as). Amesema kuwa nchi au kundi lolote linalotaka kujitawala na kuwa huru halikubaliwi katika siasa za Marekani. Amesema tawala za Kiarabu zimepigishwa magoti na Marekani na kwamba hazina uwezo hata wa kupanga bei ya mafuta zinayoyazalisha zenyewe.
Sayyid Nasrallah amesema Israel ni wenzo na chombo kinachotumiwa na Marekani na waitifaki wake kwa ajili ya kudhibiti nchi za Kiislamu na eneo la Mashariki ya Kati na kwamba sera za Marekani hazitaki kuwepo nchi imara na yenye nguvu katika eneo hilo. Amesema, kwa sababu hiyo, Marekani inaanzisha vita vya kisiasa, kipropaganda na kiuchumi dhidi ya nchi au upande wowote unaoupinga utawala wa Kizayuni wa Israel.
Katibu Mkuu wa Hizbullah pia amepinga madai ya Marekani eti ya kutetea demokrasia na haki za binadamu akisema, nchi hiyo inawaunga mkono na kuwasaidia watawala madikteta wakubwa na wanaovunja na kukanyaga haki za binadamu na vilevile nchi ambazo hazina hata katiba au chaguzi za kidemokrasia. Amesema kuwa vita vinavyoendelea sasa nchini Syria na katika nchi kama Yemen ni sehemu ya siasa za Marekani za kudhibiti na kuzipigisha magoti nchi zote zinazopinga sera za Washington na waitifaki wake na kwamba makamanda wa kweli wa vita hivyo si Abu Bakar al Baghdadi, Aiman al Dhawahiri au Mfalme Salman bin Abdul Aziz wa Saudia bali ni Marekani yenyewe.
Sayyid Hassan Nasrallah ameashiria uongo wa Marekani kuhusu miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia nchini Iran na kusema: Inasikitisha kwamba nchi za Kiarabu zililivalia njuga suala hilo kuliko hata Wamarekani wenyewe lakini Iran ilisimama ngangari na kudumisha shughuli zake katika uwanja huo hadi Marekani ikalazimika kufanya mapatano na Tehran.../mh

3393060

captcha