Katika maandamano hayo yaliyofanyika katika miji ya Lafia, Katsina, Kaduna na Gombe, Waislamu wa Nigeria walibeba mabango ya picha za Sheikh Zakzaky na Waislamu wengine waliouliwa au wanaoendelea kushikiliwa na jeshi la Nigeria. Waandamanaji hao wamelaani kuendelea kuwekwa kizuizini Sheikh Zakzaky na kutaka kiongozi huyo pamoja na mamia ya Waislamu wengine walioko kizuizini waachiliwe huru haraka iwezekanavyo na bila ya masharti yoyote.
Mnamo tarehe 12 Desemba mwaka jana, askari wa jeshi la Nigeria waliwashambulia Waislamu waliokuwa kwenye mjumuiko wa kidini katika kituo cha Kiislamu kilichoko kwenye mji wa Zaria kwa madai kuwa walizuia msafara wa mkuu wa majeshi na kufanya jaribio la kutaka kumuua.
Siku iliyofuata wanajeshi hao walivamia nyumba ya Sheikh Ibrahim Zakzaky na kumtia nguvuni baada ya kuwapiga risasi na kuwaua wale waliojaribu kumhami kiongozi huyo akiwemo kiongozi mmoja mwandamizi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria pamoja na msemaji wa harakati hiyo.
Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limesema watu wasiopungua 300 waliuliwa katika matukio mawili hayo wakiwemo watoto watatu wa kiume wa Sheikh Zakzaky, huku Amnesty International ikuelezea ukatili uliofanywa na jeshi la Nigeria kuwa ni wa "kutisha".
Tume ya Kiislamu ya Haki za Binadamu (IHRC) yenye makao yake London, Uingereza imesema kuna ushahidi wa kuaminika kuwa jeshi la Nigeria lilizizika kwa siri kwenye makaburi ya halaiki maiti za mamia ya Waislamu waliouliwa wakati wa uvamizi kwenye nyumba ya Sheikh Zakzaky.