Wanawake wanaohudumu katika Shirika la Ndege la Air France wamefahamishwa kuwa ni sharti wavae Hijabu wakati ndege yao inaposimama nchini Iran.
Christophe Pillet mkuu wa jumuiya ya wafanyakazi Air France amesema ndege za shirika hilo zinaanza safari za Tehran mwezi huu wa Aprili baada ya kuondolewa vikwazo. Ameongeza kuwa, wafanyakazi wa kikeo wanaohudumu katika ndege hiyo wamefahamishwa kuwa watakapoondoka nje ya ndege wakiwa katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wanatakiwa kuwa na mavazi yenye kufunika miguu yao na pia wavae mtandio kichwani. Shirika la Air France limesema lina heshimu sheria hiyo ya Iran kuhusu Hijabu na litwachukulia hatua kali wafanyakazi wake watakakaokiuka sheria hiyo. Wakuu wa Air France wamesema kwa kuzingatia kuwa raia wote wa kigeni wanaotembelea Iran wanazingatia sheria ya vazi la stara la Hijabu, wahudumu wa ndege pia wanapaswa kutii sheria hiyo. Shirika la Air France linarudi Iran baada ya kukatiza safari zake nchini mwaka 2008 kufuatia vikwazo vya kimataifa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.